Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwezi wa Ramadhani ni fursa isiyokuwa na mbadala kwa ajili ya kutubu madhambi, kutakasa nafsi na kuzingatia takwa na ucha-Mungu katika masuala ya kijamii na kisiasa. Ametilia mkazo udharura wa kuwepo umoja na mshikamano na akasema: "Umoja kati ya viongozi wa mfumo wa Kiislamu ni wajibu mkubwa na kufanya juhudi za kuvuruga umoja huo ni kinyume cha sheria za dini."
Ayatullah Khamenei amesema kuwa mwezi wa Ramadhani katika kila mwaka ni sawa na fursa za swala katika kila usiku na mchana; ni fursa ya kuzinduka, kunong'ona na Mola na kutia nuru katika moyo na nafsi.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa toba na kurejea kwa Mola ni miongoni mwa sifa makhsusi na muhimu mno kati ya sifa za mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ameashiria pia wajibu mzito wa viongozi na wafanyakazi katika uwanja huo na kuongeza kuwa kuacha njia, fikra na kazi isiyokuwa sahihi na kurejea kwa Mwenyezi Mungu kunahitajia kwanza kutambua tatizo na makosa yenyewe.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uwanja wa kutubia madhambi na kurejea kwa Mola katika masuala yote ya mtu binafsi na jamii ni mkubwa na akaongeza kuwa watu wote wenye taathira katika nyanja mbalimbali za jamii wanapaswa kuchunga nafsi zao wenyewe, taasisi wanazosimamia na maneneo yanayoathiriwa na maneno na mwenendo wao, kwani iwapo makosa ya taasisi hizo yatategemea mwenendo na maneo ya kiongozi wake hapana shaka yatanasibishwa kwa kiongozi huyo.
Amesema kuwa lengo la kutubu na kusahihisha fikra na amali ni kupata takwa na ucha-Mungu. Ameongeza kuwa ni muhimu kuchunga takwa, kuacha mambo ya haramu na kutekeleza wajibu wa mtu binafsi, lakini takwa ina sehemu nyingine muhimu zaidi ambayo mara nyingine inapuuzwa.
Ayatullah Ali Khamenei amedondoa vipengee vya dua tukufu ya Makarimul Akhlak iliyoko katika kitabu cha Sahifa Sajjadiyyah, na akesema kuwa kueneza uadilifu, kuinamisha chini macho, kusuluhisha uhasama, kujenga umoja, kuzima moto unaochochewa katika jamii na kukutanisha pamoja watu waliojitenga na majmui ya waumini kwa sababu moja au nyingine ni sehemu muhimu mno ya takwa na ucha-Mungu. Ameongeza kuwa hayo ni miongoni mwa masuala muhimu ya jamii yetu ya sasa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sehemu muhimu zaidi ya takwa na ucha-Mungu ni kufanya juhudi za kueneza uadilifu katika nyanja zote. Amesema uadilifu katika utekelezaji na masuala ya kijamii, uadilifu katika kugawa utajiri na fursa mbalimbali na uadilifu katika kuchagua watu kwa ajili ya kazi mbalimbali ni miongoni mwa vielelezo vya uadilifu kwa maana yake halisi.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kuzuia hasira zinazozusha upotofu katika fikra na matendo ni sehemu nyingine ya takwa na ucha-Mungu. Ameashiria umuhimu wa kukabiliana na kuondoa hitilafu na akasema: "Baadhi ya watu wanachochea moto wa hitilafu wa kisiasa kati ya mirengo na watu mbalimbali na kukabiliana na harakati hizo ni katika vielelezo vya takwa na ucha-Mungu."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena juu ya udharura wa kuvutia idadi kubwa zaidi ya watu na kusukumia mbali idadi ndogo zaidi kama sehemu ya siasa kuu za Iran na akasema kuwa kigezo na kipimo cha jambo hilo ni misingi na thamani zetu; hata hivyo tunapaswa kutambua kwamba imani za watu zina daraja tofauti na watu waliojitenga kutokana na makosa au mghafala wanapaswa kurejeshwa kwenye njia kwa kutumia nasaha na hoja.
Ayatullah Khamenei amesema ibada ya funga ni amali ya pamoja inayofanywa na jamaa na kuongeza kuwa iwapo watu wote wanaoketi kwenye meza yenye baraka tele ya mwezi wa Ramadhani, yaani taifa la Iran na mataifa mengine ya Kiislamu, yatatumia fursa hiyo kwa ajili ya kutubu na kurejea kwa Mwenyezi Mungu, basi maswala yote ya ndani na matatizo ya umma wa Kiislamu yatapatiwa ufumbuzi. Inandelea.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya umuhimu wa kutiliwa maanani uhakika wa mambo kati ya kambi mbili za taifa la Iran na kambi ya ubeberu kwa ajili ya kuweza kuchambua kwa njia sahihi masuala ya ndani na ya nje. Amesema kuwa uchunguzi wa kina kuhusu mpambano wa kambi hizo mbili katika kipindi cha miaka 32 iliyopita unaonesha kwamba taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu imedumisha njia, misingi na malengo yale yale ya Mapinduzi na Imam Khomeini ilhali kambi ya ubeberu imekumbwa na mabadiliko.
Ayatullah Khamenei amesema kambi ya maadui wa taifa la Iran inaendelea kudhoofika huku Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikistawi na kuimarika zaidi. Ameongeza kuwa ingawa kambi inayokabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasema urongo mkubwa kwa kudai kuwa ndiyo jamii ya kimataifa, lakini utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani tu ndio mhimili wa kambi hiyo.
Akifafanua zaidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria maana mbili za upinzani wa kijujuu na upinzani wa kimsingi na akasema kuwa upinzani wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya Iran ni upinzani wa kimsingi.
Ameongeza kuwa: "Upinzani wa kimsingi ni upinzani dhidi ya kuwepo kwa Jamhuri ya Kiislamu, na kama ambavyo sisi tunautambua utawala wa Kizayuni kuwa ni utawala ghasibu na bandia na unaoelekea kuangamia, nao pia unapinga kuwepo kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Akibainisha upinzani wa kimsingi kati ya Iran na Marekani, Ayatullah Khamenei amesema, mtazamo wa Wamarekani kwetu sisi ni mtazamo unaopinga asili ya kuwapo mfumo wa Kiislamu licha ya madai yao ya kutaka eti kufanyika mabadiliko katika mwenendo wa Jamhuri ya Kiislamu; vivyo hivyo sisi pia tunapinga ubeberu na ujuba wa Marekani.
Ayatullah Khamenei pia ameeleza vielelezo vya mwenendo wa kudhoofika kambi ya maadui wa taifa la Iran na akaashiria hali ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani ya kutokuwa na uungaji mkono wa watu duniani. Amesema: "Chuki ya mataifa mbalimbali dhidi ya tawala hizo mbili, kufeli kwao katika matukio ya kijeshi ya miaka ya hivi karibuni huko Iraq, Afghanistan na Palestina, matatizo ya mdororo mkubwa wa kiuchumi, kufeli siasa zao kuhusu Mashariki ya Kati katika nchi za Syria, Lebanon na Palestina, kupungua kwa hali ya kujiamini viongozi wa Marekani na Israel na kushindwa Marekani katika kuchukua maamuzi kama ya kuendelea kuzikalia kwa mabavu au kuondoka katika nchi za Iraq na Afghanistan ni mifano ya wazi ya mwenendo wa kudhoofika kambi ya maadui wa taifa la Iran."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia ameeleza sababu za kupanda juu na ustawi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiashiria maendeleo mbalimbali katika medani ya sayansi na teknolojia. Amesema kuwa mbali na harakati inayong'ara katika medani mbalimbali, taifa la Iran pia lina ari na moyo aali wa kitaifa katika masuala ya kijamii na kiroho, na kwamba suala la kuhudhuria wananchi milioni 40 katika uchaguzi wa mwaka uliopita wa rais ni kielelezo cha nishati na harakati kubwa ya kijamii na kisiasa hapa nchini.
Akizungumzia suala hilo, Ayatullah Khamenei ameashiria uungaji mkono usiokuwa na kifani wa mataifa ya Kiislamu kwa Jamhuri ya Kiislamu. Ameashiria mapokezi yanayofanywa na mataifa mbalimbali kwa ajili ya kuwakaribisha viongozi wa Iran ya Kiislamu waliotembelea nchi mbalimbali katika kipindi chote cha miongo mitatu iliyopita na akasema: "Taifa la Iran lenye uzoefu uliofanikiwa wa kisiasa katika Mashariki ya Kati na maeneo mengine duniani na lenye matumaini na mustakbali litaendeleza harakati yake, na suala hilo linathibitisha harakati inayostawi na kukua ya Jamhuri ya Kiislamu."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya udharura wa kutafakati, tadbiri na kuweka mikakati mizuri kwa ajili ya kukabiliana na kambi ya maadui. Amesema kuwa maadui hao pia wanapanga mikakati dhidi yetu, kwa msingi huo tunapaswa kushikamana na kusonga mbele kwa kutegemea akili, busara na ushujaa katika medani hiyo.
Akifafanua zaidi mipango ya maadui wa kigeni, Ayatullah Khamenei amezungumzia pia mashinikizo ya kiuchumi, vitisho vya mashambulizi ya kijeshi, vita vya kisaikolojia, machafuko ya kisiasa na uharibifu unaofanywa na maadui hao hapa nchini. Amesema kuwa sambamba na mipango hiyo yote yaani kuweka vikwazo, kutoa vitisho na kupasisha maazimio dhidi ya Iran, Wamarekani wanadai kwamba wako tayari kuketi kwenye meza ya mazungumzo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Wamarekani wamekuwa wakitumia mbinu hizo zote katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita na akaongeza kuwa: "Vikwazo vya miaka 30 dhidi ya Iran, vitisho vya siku zote katika kipindi cha utawala wa marais tofauti wa Marekani, propaganda chafu zisizosita dhidi ya Imam Khomeini na taifa la Iran na uharibifu na machafuko yanayofanywa katika baadhi ya vipindi na vibara wao wa ndani, vinaonesha kwamba Marekani bado inatumia mbinu zilizochakaa katika kukabiliana na taifa la Iran."
Amesema kuwa tangazo la Marekani kwamba iko tayari kufanya mazungumzo na Iran ni madai ya kukaririwa. Amepinga suala la kufanyika mazungumzo ya aina yoyote chini ya vitisho na siasa za kutumia mabavu na akasema: "Iran imefanya mazungumzo na Marekani katika masuala mawili yaani kuhusi Iraq na suala jingine ambayo tunayatambua kuwa miongoni mwa masuala muhimu ya kiusalama; hata hivyo uzoefu umeonesha kwamba mara zote wanapokabiliana na hoja madhubuti katika meza ya mazungumzo, Wamarekani wamekuwa wakitumia lugha ya mabavu na kukata mazungumzo kwa upande mmoja."
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Iran imekataa kufanya mazungumzo na Marekani kwa hoja za wazi kwa sababu haiyatambui mazungumzo yanayofanyika chini ya kivuli cha vitisho, mashinikizo na kutia hofu kuwa ni mazungumzo kweli; kwa sababu hiyo na kama viongozi wa nchi walivyosema, sisi ni watu wa mazungumzo lakini si pamoja na Wamarekani wanaotaka kufanya mazungumzo chini ya kivuli cha vitisho, vikwazo na sera za kutumia mabavu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kama Wamarekani watateremka chini kutoka kwenye ngazi iliyochakaa ya kujiita dola kubwa, wakaweka kando vitisho na vikwazo na kuainisha lengo la mazungumzo, sisi pia kama tulivyosema huko nyuma, tuko tayari kuketi kwenye meza ya mazungumzo; hata hivyo wao si watu wa mazungumzo na wanataka kutumia mabavu tu.
Akiendeleza mjadala huo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Wamarekani wanapaswa kutambua kwamba hawawezi kuiwekea mashinikizo Iran kama wanavyozifanya nchi nyingine kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu haikubali mashinikizo ya aina yoyote na itajibu mashinikizo hayo kwa kutumia mbinu zake.
Kuhusu suala la kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza tena kuwa suala la kurutubisha madini ya urani ni haki ya taifa la Iran. Amesema taifa na viongozi wa Iran hawatalegeza kamba katika kutetea haki hiyo na watatekeleza haki yao kwa kujenga vituo zaidi vya nyuklia na kuzalisha nishati hiyo ndani ya nchi.
Amesema kuwa baadhi ya matamshi yanayotolewa na Wamarekani kuhusu suala la kudhamini fueli ya nyuklia inayohitajika hapa nchini hayana maana yoyote. Amezungumzia urongo wa madola ya kigeni kuhusu kadhia ya kudhamini nishati iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 kwa ajili ya kituo cha nyuklia cha Tehran na akaongeza kuwa: "Kwa mujibu wa kaida zinazotumika katika miamala mbalimbali duniani Iran ilinunua nishati ya kituo hicho miongo miwili iliyopita lakini pale Wamagharibi walipohisi kwamba Tehran inahitajia nishati hiyo iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 walianza mchezo mchafu na makosa hayo makubwa ya Marekani na nchi za Magharibi yamekuwa na madhara kwao wenyewe.
Amesema moja ya matokeo ya mchezo huo mchafu wa nchi za Magharibi ni kuihamasisha Iran kuzalisha yenyewe nishati ya nyuklia iliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia 20 na kuthibitika kwamba Marekani na nchi nyingine zinazozalisha nishati hiyo haziwezi kuaminiwa. Amesisitiza kuwa kadhia hii imeyaonesha mataifa yote kwamba nchi hizo haziwezi kuaminiwa kabisa.
Kuhusu vitisho vya kuishambulia kijeshi Iran vinavyotolewa na Marekani, Ayatullah Ali Khamenei amesema ni jambo lililo mbali kwa Wamarekani kufanya upumbavu kama huo lakini dunia nzima inapaswa kuelewa kwamba iwapo vitisho hivyo vitatekelezwa basi medani ya mapambano ya taifa la Iran haitaishia katika eneo hili pekee bali itakuwa kubwa zaidi.
Vilevile Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezitaja propaganda chafu na madai ya Marekani ya kukiukwa haki za binadamu nchini Iran kuwa ni kichekesho. Ameongeza kuwa kama walivyoonyesha huko Iraq, Afghanistan na Palestina, Wamarekani hawathamini hata kigodo uhai wa mwanadamu hata hivyo wanazungumzia bila haya suala la eti ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia hatua madhubuti zilizochukuliwa na viongozi wa Iran ya Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na mipango ya adui ikiwa ni pamoja na vikwazo vyao vya kiuchumi na akasema kuwa viongozi wa mfumo wa Kiislamu hapa nchini wamechukuwa maamuzi sahihi mno ya kukabiliana na maazimio ya vikwazo na vikwazo vya upande mmoja vya Marekani na nchi za Ulaya na kwa matakwa yake Allah na chini ya kivuli cha umoja na mshikamano, vikwazo hivyo vitakuwa fursa kwa taifa la Iran.
Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya umuhimu wa kuzidishwa na kuboreshwa uzalishaji wa taifa katika medani hiyo na akaongeza kuwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje unapaswa kudhibitiwa na kama kuna haja ya kupasishwa sheria kuhusu kadhia hiyo Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge) inapaswa kuchukua hatua hiyo.
Aidha ametilia mkazo udharura wa kutumia akili, busara na ushujaa katika kukabiliana na mipango ya adui na akasema kuwa tunapaswa kudumisha njia yetu kwa ushujaa, busara, azma kubwa na bila ya kutetereka.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa umoja na mshikamano ni nguzo imara ya taifa na mfumo wa Kiislamu katika kudumisha harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa umoja na mshikamano wa viongozi wa nchi ni wajibu na hatua yoyote ya kupinga umoja huo hususan katika uongozi wa juu ni kinyume cha sheria za dini.
Ameashiria pia njama za maadui za kutilia chumvi hitilafu ndogo ndogo na kuzidhihirisha kuwa ni kubwa na akasema hitilafu za kimitazamo kati ya serikali na bunge si maafa, lakini kuzifanya hitilafu hizo kuwa ufa na migawanyiko isiyoweza kurekebishwa na majeraha yasiyotibika ni makosa makubwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa siku kadhaa zilizopita alilitaka Baraza la Kulinda Katiba kuingilia kati masuala yanayozusha mjadala kati ya bunge na serikali ili liweze kutatua masuala hayo kwa kuainisha mipaka ya mamlaka na wajibu wa kila taasisi na kutekeleza kipengee cha Katiba cha kujitegemea nguvu tatu za dola.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo udharura wa kushikamana na kulinda misingi na kutocheza katika uwanja wa adui. Amesema kuwa adui anafanya njama za kuharibu imani ya wananchi kwa viongozi na kwamba wananchi wote wanapaswa kujiepusha kusema maneno yanayovunja imani ya wananchi kwa Serikali, Bunge la Chombo cha Sheria.
Vilevile amekosoa wale wanaoshuku bila ya hoja takwimu zinazotolewa na vyombo husika na akasema kuna udharura wa kujiepusha na vitendo vinavyodhoofisha imani ya wananchi.
Mwishoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa yote yaliyosemwa yanawezekana tu chini ya rehma na huruma yake Mola Muweza na kuwa na matumaini na ahadi yake. Amesisitiza kwamba taifa la Iran kama ilivyokuwa huko nyuma litadumisha njia hiyo iliyojaa fahari kwa kutegeme maswala hayo.
Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran pia amehutubia hadhara hiyo akitoa ripoti ndefu kuhusu shughuli na juhudi zilizofanywa na serikali katika nyanja mbalimbali za kiutamaduni, kiuchumi, sayansi na teknolojia, ujenzi, viwanda, madini, marekebisho ya muundo wa idara, siasa za nje na uendeshaji wa masuala ya ndani.
Rais Ahmadinejad amesema kuwa masuala ya kiutamaduni ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele mno na serikali. Ameashiria malengo ya kiutamaduni ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa serikali imezidisha bajeti ya masuala ya kiutamaduni mara tatu zaidi.
Katika upande wa masuala ya sayansi na teknolojia, Rais Ahmadinejad amesema kuwa serikali imezidisha bajeti ya masuala ya utafiti na kutekeleza mpango wa mageuzi katika sekta ya elimu. Vilevile ameashiria maendeleo makubwa ya sekta ya afya na tiba na akasema kumepatikana maendeleo makubwa katika teknolojia ya masuala ya anga na kwamba satalaiti mpya ya Iran itarushwa angani hivi karibuni. 636835