Kasisi mwenye misimamo mikali wa Kimarekani Terry Jones amelazimika kufuta uamuzi wake wa kutaka kuchoma moto nakala za kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwa mnasaba wa kumbukumbu ya Septemba 11, baada Waislamu ulimwenguni kuungana katika kulaani uamuzi huo.
Mashekhe na maimamu wa Sala za Idul-Fitr iliyosaliwa Ijumaa na Jumamosi katika maeneo mbalimbali ulimwenguni walilaani wito wa kasisi huyo na kuutaja kuwa ni dharua ya hali ya juu. Aidha mabaraza ya idi yaliyofanyika baada ya Sala ya Idul Fitr nayo yalitawaliwa na wito wa kulaani kitendo cha kasisi huyo wa Kimarekani.
Baraza Kuu la Waislamu Tanzania kupitia Mufti Mkuu Issa Shaaban bin Simba limelaani kitendo hicho na kusisitiza kuwa, kampeni hizo haramu zinalenga moja kwa moja kuutukana Uislamu na Waislamu kote duniani, hivyo hawatakubali kunyamaza na kuangalia matusi hayo ambayo yanaweza kusababisha vurugu duniani kote.
Viongozi wa Kiislamu nchini Kenya wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Sheikh Mohammad Dor wamelaani vikali mpango wa kasisi Jones. Wameutaka ubalozi wa Kenya mjini Washington kuwasilisha malalamiko ya Waislamu wa Kenya kwa serikali ya Marekani.
Nchini Afghanistan maandamano makubwa ya kumlaani kasisi huyo yameshuhudiwa ambapo waandamanaji hao wamesikika wakipiga nara dhidi ya maadui wa Uislamu. Maandamano kama hayo yameshuhudiwa pia katika nchi mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu.
652332