Akizungumza hivi karibuni katika Msikiti wa Imam Swadiq (as) katika mji wa Diraz Ayatullah Isa Qassim amesema kuwa tukio la Karbala lilisimamishwa na Imam Hussein (as) kwa ajili ya kuuokoa Uislamu, kuwaokoa watu kutokana na tamaa ya dunia, kuwarejesha Waislamu kwenye dini na kuleta mwamko kwenye umma wa Kiislamu. Amesema kwa msingi huo, Waislamu wanapasa kujivunia kujitolea kwa Imam Hussein katika siku ya Ashura na kuiheshimu siku hiyo.
Ayatullah Isa Qassim amesema hii inatokana na ukweli kwamba Imam Hussein (as) aliuokoa Uislamu kutokana na hatima nyeusi na upotofu mkubwa.
Ayatullah Sheikh Isa Qassim amewasihi Waislamu kunufaika na Qur'ani Tukufu katika kutambua haki na batili kwa sababu kitabu hicho kitakatifu kimejaa aya zinazozungumzia na kuunga mkono msimamo aliouchukua Imam Hussein katika ardhi ya Karbala na kulaani vitendo vya dhulma na upotofu wa Yazid.
Amesema ni wazi kuwa Imam Hussein aliishi kwa msingi wa mafundisho ya Qur'ani Tukufu jambo ambalo amesisitiza hakuna mtu yoyote anayeweza kulithibitisha kuhusiana na dhalimu kama Yazid. Ameshangaa ni kwa nini watawala wa Bahrain wamechukua msimamo wa kupiga marufuku mambo yanayoeneza fikra safi za Imam Hussein (as) katika jamii na kuruhusu mabango na picha chafu zinazohubiri ufuska na utovu wa maadili kuenea katika mitaa ya nchi hiyo.
Ayatullah Isa Qassim amesema kuwa kitendo hicho ni dhulma kubwa kwa Imam Hussein (as) na uhuru wa kuabudu. Ameongeza kuwa jambo hilo ni dharau kwa nembo za kidini na kimadhehebu za raia na kwamba litachochea fitina miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo. 710930