Mufti wa Syria amewaambia viongozi wa Vatican kwamba hakuna haja ya wao kuwa na wasiwasi kuhusu Wakristo wanaoishi katika nchi za Kiislamu kwani Uslamu unawalinda na Vatican inapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu hali ya watu wanaoishi katika ardhi za Palestina na miinuko ya Golan chini ya ukandamizaji wa utawala ghasibu wa Israel na makundi yenye misimamo mikali ya Kiyahudi.
Sheikh Ahmad Badruddin Hassoun ameashiria azimio lililotolewa na maaskofu wa Kanisa Katoliki kuhusu udharura wa kulindwa Wakristo wanaoishi Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa suala hilo halikuwa na udharura wowote na kwamba Waislamu na Wakristo wanaoishi katika nchi za Kiislamu wanaishi kama ndugu wa familia moja na wanashirikiana katika masuala mengi ya kidini na kitaifa.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake, Mufti wa Syria ameitaka Vatican kuwa na waswasi kuhusu maisha ya watu wanaoishi chini ya ukandamizaji wa Israel inayoendelea kufanya mikakati ya kuimarisha dola la kibaguzi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Amekaribisha mpango wa Syria wa kuitisha kongamano la kimataifa la mazungumzo kati ya Uislamu na Ukristo na akasema mazungumzo hufungua njia ya kuondoa hitilafu na kuimarisha ushirikiano. 712661