IQNA

Sisitizo la kudhaminiwa usalama na hali nzuri kwa waombolezaji wa Arabaini ya Imam Hussein (as)

13:30 - January 09, 2011
Habari ID: 2061201
Huku akiashiria kuanza kwa misafara ya waombolezaji wa Imam Hussein (as) wanaotembea kwa miguu kuelekea katika mji mtakatifu wa Karbala kwa madhumuni ya kushiriki katika Arbaini ya mjukuu huyo wa Mtume (saw), hatibu wa swala ya Ijumaa ya mjini Kadhimain nchini Iraq amesisitiza juu ya udharura wa kudhaminiwa hali bora na usalama wa wafanyaziara hao katika siku hizi tukufu.
Hujjatul Islam wal Muslimeen Jalal ad-Deen Swaghir amesema kuwa kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita, tayari wakazi wa mikoa ya kusini mwa Iraq wameanza kutembea kwa miguu kuelekea Karbala kwa lengo la kushiriki katika Arbaini ya Imam Hussein (as) ambayo huhudhuriwa na mamilioni ya wapenzi wa mtukufu huyo na Watu wa Nyumba ya Mtume (saw).
Sheikh Jalal ad-Deen amesema misafara hiyo ya mamilioni ya watu huwashangaza walimwengu ambao hustaajabu jinsi Mashia walivyo na mapenzi makubwa kwa Imam Hussein na Watu wote wa Nyumba ya Mtume (saw). Sheikh Swaghir amesema kuwa umati huo mkubwa wa wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume huwafanya walimwengu kujiuliza maswali mengi na kufanya utafiti kuhusu tukio la Karbala na sababu ya kuuawa shahidi Imam Hussein na hatimaye kufikia ukweli kuhusu suala hilo.
Imam huyo wa swala ya Ijumaa ametaka kuandaliwa suhula za kutosha kwa ajili ya umati huo mkubwa wa mamilioni ya watu na kuelezea matumaini yake kwamba vyombo husika ikiwemo Idara ya Wakfu, Hilali Nyekundu ya Iraq na wasimamizi wa makundi ya maombolezo ya Imam Hussein (as) vitachukua hatua za lazima kuhakikisha kwamba waombolezaji wanatekeleza ibada hiyo kwa njia ifaayo.
Sheikh Swaghir pia ameridhishwa na mwenendo wa kukarabatiwa haram ya Imam Musa Kadhim (as). 726328
captcha