Sheikh Muhammad al-Ibad, mwanafikra na hatibu mashuhuri wa Kishia wa Saudi Arabia amesema kuwa kuwepo mshikamano na umoja wa madhehebu ya Kiislamu kunaweza kuzuia uingiliaji wa wageni katika masuala ya ndani ya ulimwengu wa Kiislamu.
Amezitaka nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kutambua rasmi na kuamiliana kwa usawa na madhehebu yote ya Kiislamu ili kutatua matatizo mengi yanayozikabili nchi hizo yakiwemo matatzio ya kimadhehebu.
Akizungumza katika Msikiti wa Imam Swadiq (as) katika mkoa wa Ahsaa, msomi huyo wa Kiislamu amesema kuwa kufumbiwa macho ukweli wa kuwepo madhehebu tofauti ya Kiislamu katika nchi za Kiarabu ni jambo ambalo halitatatua tatizo lolote bali litaendelea kuharibu zaidi hali ya mambo katika nchi hizo, na hivyo kuzishawishi nchi za kigeni kuingilia masuala ya ndani ya ulimwengu wa Kiislamu. Amesema kushirikishwa wafuasi wa madhehebu tofauti katika uendeshaji wa nchi kupitia idara tofauti za serikali ni hatua muhimu katika utatuzi wa fitina za kimadhehebu katika nchi za Kiarabu.
Ameelezea matumaini yake kwamba taasisi muhimu za kukurubisha pamoja madhehebu ya Kiislamu kama ile iliyoko nchini Iran zitaanzishwa katika nchi za Kiarabu ili kufikia lengo hilo muhimu. 797113