IQNA

Ayatullah Khamenei:

Wajibu wa wanachuo vijana ni kudumisha njia ya Mapinduzi ya Kiislamu

9:58 - August 11, 2011
Habari ID: 2168811
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mapinduzi makubwa ya taifa la Iran yalifanyika kwa malengo maalumu na yakiwa kama tukio la aina yake katika historia, yangali yanafuatilia malengo na thamani hizo bila ya kupotoka na kuyumba.
Ayatullahil Udhma Ali Khamenei aliyasema hayo jana usiku katika hadhara ya mamia ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wawakilishi wa jumuiya za kielimu, kiutamaduni na kisiasa nchini Iran. Amefafanua mwenendo wa kupotoka mapinduzi mbalimbali duniani na kueleza uthabiti na kudumu kwa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Amesema miongoni mwa malengo makuu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kupigania Uislamu, kupambana na ubeberu, kulinda uhuru na kujitawala kwa taifa, kumrejeshea mwanadamu hadhi na heshima yake, kuwatetea wanaodhulumiwa na maendeleo na ustawi wa pande zote wa Iran ya Kiislamu.
Amesema kuwa matakwa na maneno ya kizazi cha sasa cha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran yamepevuka zaidi, yamepimwa na ni ya kitaalamu zaidi kuliko yale ya kizazi cha mwanzoni mwa Mapinduizi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa hisia za vijana wa sasa ndizo zile zile za vijana wa kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu lakini vijana wa sasa wamekuwa na busara na hikima zaidi, suala ambalo lina thamani kubwa.
Akifafanua jinsi Mapinduzi ya Kiislamu yalivyojizatiti na kujitegemea, Ayatullah Khamenei ameashiria upotofu ulioyakumba mapinduzi na harakati kubwa za wananchi katika karne za hivi karibuni na hatima yao na akasema mapinduzi makubwa ya Ufaransa ni mfano wa wazi wa mapinduzi makubwa ya wananchi yaliyofanyika dhidi ya utawala wa kisultani wa zama hizo, lakini mapinduzi hayo yalijitenga na malengo ya awali ya wananchi kadiri siku zilivyosonga mbele na mwishowe, baada ya mashaka mengi, mfumo wa kisultani ulitawala tena nchini Ufaransa.
Ayatullahil Udhma Ali Khamenei ameutaja uhuru wa Marekani na kuasisiwa nchi hiyo kama kielelezo kingine cha harakati za wananchi ambazo zilijitenga na malengo yake ya awali kadiri miaka ilivyopita na kukumbwa na migogoro ya vita na mauaji ya wao kwa wao.
Vilevile ametaja baadhi ya mapinduzi ya mwishoni mwa mwongo wa 50 na mwanzoni mwa mwongo wa 60 Miladia katika mashariki ya Kati, kaskazini mwa Afrika na America ya Latini kama mifano mingine ya mapinduzi yaliyopotoka na kujitenga na malengo yake ya awali na akasema: “Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni tukio la aina yake katika kipindi chote cha miaka mia moja iliyopita, kwani yameweza kulinda na kufuatilia malengo na misingi yake ya awali kwa nguvu, bila ya kuyumba na kwa nishati inayoongezeka kila uchao.” 841165

captcha