IQNA

Mkuu wa Baraza Kuu la Kiislamu Iraq:

Viongozi wa nchi mbalimbali wajifunze kutokana na hatima ya Gaddafi

17:42 - August 24, 2011
Habari ID: 2176401
Kiongozi wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq Sayyid Ammar Hakim amewapongeza wananchi wa Libya kwa kupata ushindi dhidi ya dikteta wa nchi hiyo na kusema viongozi wa nchi za Mashariki ya Kati wanapaswa kupata ibra na funzo kutokana na hatima ya dikteta wa Libya.
Taarifa iliyotolewa na Sayyid Ammar Hakim imesema kuwa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq limemtumia ujumbe Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Libya Mustafa Abduljalil likimpongeza yeye na wanamapinduzi wa nchi hiyo kwa kupata ushindi dhidi ya dhulma za zaidi ya miaka 40 za Muammar Gaddafi.
Taarifa hiyo imesema, matunda ya mapinduzi ya wananchi wa Libya na yale yaliyojiri kwenye medani ya mapambano dhidi ya dikteta wa nchi hiyo ni tukio muhimu katika historia ya sasa. Ammar Hakim ameongeza kuwa yaliyotokea Libya yanapaswa kuwa ibra na somo kubwa kwa watu wote.
Amesisitiza kuwa somo hilo limetoa ibra kubwa hususan baada ya yaliyotokea katika nchi za Iraq, Misri na Tunisia.
Kiongozi wa Baraza Kuu la Kiislamu la Iraq amewataka wanamapinduzi wa Libya kuimarisha umoja, udugu na mshikamano wao na kuweka kando hitilafu na migawanyiko. 849289

captcha