IQNA

Maisha ya Imam Ja'afar Sadiq AS

14:05 - September 22, 2011
Habari ID: 2191884
Tarehe 25 Shawwal mwaka 148 Hijria Qamaria, Ulimwengu wa Kiislamu ulitumbukia katika msiba mkubwa kutokana na kumpoteza Imam Sadiq AS kutoka Ahlul Bayt wa Mtume SA. Katika siku hii Imam Ja’afar Sadiq AS akiwa na umri wa miaka 65 alifikia daraja ya shahada baada ya kupewa sumu kwa amri ya Mansur Dawaniqi, Khalifa wa Pili wa silisili ya Makhalifa wa Bani Abbas.
Makala hii itaangazia kwa kifupi maisha ya Imam Sadiq AS.
Katika maisha yaliyojaa baraka ya Imam huyu mtukufu kuna masuala mawili ambayo yanahusiana na kuwa na mfungamao wa moja kwa moja. La kwanza ni kupambana na dhulma na madikteta wa zama na jingine ni kuuarifisha Uislamu halisi pamoja na kuonyesha uso wa kweli wa dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Katika kipindi chote cha miaka 34 ya Uimamu wake, alipinga utaghuti kwa upande mmoja na kwa upande wa pili kuibua mapinduzi ya kiutamaduni katika fikra za wanaadamu kwa kuuarifisha Uislamu halisi.
Katika zama za Imam Sadiq AS hali ya kisiasa na kijamii ilipelekea Mtukufu huyu kujihusisha na harakati za kiutamaduni na kisiasa. Katika kipindi cha mapambanao makali kati ya Bani Abbas na Bani Ummaya, Imam alitumia fursa hiyo, iliyokuwa mbali na mashinikizo ya kisiasa, kurekebisha na kueneza utamaduni na fikra za Kiislamu.
Suala hilo lilipelekea wapendao itikadi ya haki kote katika Ulimwengu wa Kiislamu kujumuika katika Mji wa Madina ambapo walimzunguka Imam Sadiq AS na kufaidika na nuru ya elimu yake. Kila siku idadi ya wanafunzi wa Imam iliongezeka hadi kufikia takaribani watu elfu nne. Mbinu ya Imam Sadiq AS katika kuongoza na kutangaza Uislamu ilikuwa na athari ya kina katika jamii ya zama hizo. Hata kama Imam hakutumia silaha dhidi ya mataghuti na madhalimu wa zama zake, lakini silaha yake ya elimu, kalamu na maneno ilitumika kila palipojitokeza fursa ya kupambana na dhulma. Harakati za Imam Sadiq AS za kuhubiri na kuongoza Waislamu zilifanikiwa kwa kiasi kwamba Mansour, Khalifa wa zama hizo kwa ugumu mkubwa alikiri kwa kusema hivi: “Hata kama Ja’afar bin Mohammad hasimami kwa upanga, lakini hatua anazochukua kwangu mimi ni mwamko muhimu na mkali zaidi.’
Hakuna shaka kuwa Madhehebu ya Kishia yalienea kutokana na juhudi za kielimu zisizo na kikomo za Imam Sadiq AS. Hii ndio sababu Ushia ukajulikana kama Madhehebu ya Ja’afari. Hili linaashiria nafasi muhimu ya mtukufu huyo katika kukamilisha, kuratibu na kueneza utamaduni na mafundisho ya Ahlul Bayt ambayo hadi wakati huo yalikuwa hayajasajiliwa na kuhifadhiwa.
Imam Sadiq AS kwa umakini na tadbiri maalumu aliweza kubainisha wazi masuala mbali mbali ya kiuchumi, kiibada, kimaadili, kimalezi, kifalsafa na Elmul Kalam. Alibainisha taaluma hizo kwa njia bora zaidi.
Sheikh Muhammad Abu Zahra msomi wa zama hizi wa Misri wa madhehebu ya Sunni anazungumza kuhusu shakhsia ya kielemu na kiutamaduni ya Imam Sadiq AS kwa kusema: “Maulamaa wa Kiislamu pamoja na kuwa wanahitilafiana kimitazamo, kiitikadi na kiaidiolojia, lakini wanaafikiana kimtazamo kumhusu Imam Sadiq AS, elimu na ujuzi wake."
Waandishi wa historia pia wanakiri kuhusu adhama ya shakhsia ya kielimu na ujuzi mpana wa Imam Sadiq AS.
Ibn Khalkan mwanahistoria Mashuhuri anaandika hivi: “Imam Sadiq AS ni kati ya watu wakubwa katika Ahlul Bayt wa Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW. Alipata lakabu ya Sadiq kutokana na umashuhuri wake kama mkweli katika kauli yake aidha fadhila na elimu yake ni mashuhuri kiasi cha kutohitajia ufafanuzi”.
Katika zama za Imam Sadiq AS, kuliibuka idiolojia potofu za kikafiri ambazo zilikuwa zikijishughulisha na upotoshaji jamii hasa tabaka la vijana. Imam Sadiq AS alifanya midahalao na wafuasi wa idiolojia hizo potofu. Ingawa watu hao walikuwa na uadui na chuki ya ndani dhidi ya Uislamu lakini wakati wa midahalo hiyo walikiri na kujisalimisha mbele ya dalili za nguvu za Imam. Natija ya midahalo hiyo ilikuwa ni Ummah kupata maarifa na nguzo imara katika imani ya Kiislamu.
Upana wa elimu na ujuzi wa Imam Sadiq AS haukuwa na mipaka katika taaluma kama vile Fiqhi, Usuli, Elmul Kalam, Maadili au Akhlaqi na tafsiri kwani mbali na ujuzi wa hayo, Mtukufu huyo pia alikuwa na ujuzi katika sayansi za fizikia, kemia, falaki, tiba na biolojia.
Moja ya sababu iliyopelekea makhalifa wa Kiabbasi hasa Mansour kumshinikiza na kutaka kumdhibiti Imam Ja’afar Sadiq AS ni kutokana na umashuhuri wake wa kielimu ambao ulipelekea awe na wafuasi kutoka matabaka mbali mbali ya jamii. Kwa hakika umashuhuri aliokuwa nao Imam Sadiq AS ulipelekea watawala wa Bani Abbas kuwa na uhasidi mkubwa dhidi yake. Vile vile mafundisho kuhusu siasa na serikali ya Kiislamu aliyotoa Imam Sadiq ni jambo jingine lililowakasirisha watawala wa kiimla wa Bani Abbas.
Mansour, Khalifa wa Bani Abbas alianza kuwaza namna ya kumuua shahidi Imam Sadiq AS. Lakini ukweli ni kuwa hata baada ya kuuawa shahidi mtukufu huyo si tu kuwa nuru yake yenye mwanga haikuzimika bali ilizidi kuenea na kuangaza zaidi.
Imam Sadiq AS pia alihimiza sana masuala ya maadili mema kwa wafuasi wa Ahlul Bayt. Kuhusu aliyotarajia kutoka kwa wafuasi wake, aliyabainisha kupitia mwanafunzi wake kwa kumwambia:
“Kila aliye mfuasi wetu na anayesikiliza maneneo yetu mpe salamu na mfahamishe kuwa mimi pia ninamuusia amche Mungu na atende mema, ajitahidi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kulinda amana na kuwatendea mema majirani. Hii ni kwa sababu kila mtu atayaketekeleza maelekezo haya, watu watasema yeye ni mfuasi wa Madhehebu ya Ja’afari na mimi nitafurahishwa na amali zake, lakini akifanya kinyume na hili atanisikitisha."
Moja ya nasaha za Imam Sadiq AS kwa wafuasi wake ni kuhudumiana na kusaidiana kwani suala hili hukurubisha nyoyo na kuimarisha mahusiano. Kuhusu hili Imam alisema: "Kila ambaye atachukua hatua kukidhi mahitaji ya kidini ya ndugu yake katika dini atakuwa kama mtu ambaye amepiga hatua baina ya Safa na Marwa. Mwenye Kukidhi mahitaji ya ndugu yake katika dini ni kama mtu ambaye damu yake ilimwagika kwa njia ya Mwenyezi Mungu katika vita vya Badr na Uhud. Mwenyezi Mungu haleti adhabu katika umma wowote ule isipokua unapopuuza haki za ndugu zake masikini."
Imam Sadiq AS pia aliwahimiza sana wafuasi wake kujifungamanisha na kujikurubisha na Qur’ani Tukufu. Imam alisema: "Nyumba ambayo ndani yake Qur’ani inasomwa na Mwenyezi Mungu SW anakumbukwa, baraka zake huwa nyingi na Malaika kuwa hapo na shetani kuwa mbali. Nyumba hii huonekana na watu wa mbinguni kama ambavyo nyota zinavyoonekana zikiwa zimeng'ara na watu wa ardhini."
Wapenzi wasikilizaji kwa nasaha hiyo ya Imam Ja’afar Sadiq AS ndio tunafika mwisho wa makala hii. Kwa mara nyingine tena tunatoa salamu zetu za rambirambi kwa munasaba wa kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Ja’afar Sadiq AS na tunamwomba Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe ni wenye kutekeleza Mafundisho ya Qur’ani Tukufu na vile vile tuwe wafuasi halisi wa Ahlul Bayt wa Mtume SAW.
865771

captcha