Sayyid al Satri ameyasema hayo katika mahojiano yake na kanali ya televisheni ya al Manar ya Lebanon.
Katika hali ambayo Bahrain inapita katika siku zilizogubikwa na machafuko na ukosefu wa amani huku mapinduzi ya wananchi yakiingia katika awamu mpya, Mfalme wa nchi hiyo Hamad bin Isa Aal Khalifa ameelekea Riyadh kwa ajili ya mashauriano na Mfalme wa Saudi Arabia. Safari hiyo inadhihirisha kuwa, Aal Khalifa pia ameelewa hatari iliyoko mbele yake na kuamua kukimbilia tena kwa Aal Saud kwa mashauriano zaidi. Safari tatu zilizofanywa na watawala wa Bahrain na Saudia katika miji mikuu ya nchi mbili hizo katika kipindi cha miezi sita iliyopita na pia ndoa ya kisiasa kati ya mwana wa kiume wa Sheikh Hamad Mfalme wa Bahrain na binti wa Mfalme Abdallah wa Saudi Arabia, zinaonyesha namna utawala wa Bahrain ulivyofungua akaunti mpya ya msaada wa Saudia ikiwa kinara wa nchi za Kiarabu wanachama wa Baraza la shirikiano la Ghuba ya uajemi. Saudi ni miongoni mwa nchi za Kiarabu za kandokando mwa Ghuba ya Uajemi zilizotoa msaada mkubwa wa kijeshi kwa utawala wa Aal Khalifa. Kuingia makumi ya vifaru vya nchi hiyo huko Bahrain na wakati huohuo kushiriki mamia ya vikosi vya Saudi Arabia katika kuwakandamiza na kuwauwa wananchi wa Bahrain wanaoandamana, ni ishara ya wazi ya muungano unaotia shaka kati ya viongozi wa Aal Saud na Aal Khalifa dhidi ya wananchi wa Bahrain khususan jamii ya Waislamu wa madhehebu ya ashia.
Baadhi ya wanaharakati wa kisiasa wa Bahrain wanaamini kwamba, kuweko majeshi ya Saudi Arabia nchini humo kunafanyika ili kutekeleza njama za siku nyingi za Riyadh za kutaka kuikalia kwa mabavu Bahrain kwa kushirikiana na Marekani. Saudi Arabia inajaribu kwa ghara yoyote ile kuulinda na kuubakisha madarakani utawala wa Aal Khalifa huko Bahrain baada ya kutiwa hofu na wasiwasi na kasi ya mwamko wa mapambano ya ukombozi ya wananchi wa Bahrain. Utawala wa Aal Khalifa pia ambao umetambua vyema wasiwasi wa Saudia kuhusiana na matukio yanayojiri nchini Bahrain na katika nchi nyingine za Kiarabu, unajaribu kustafidi zaidi na zaidi na uungaji mkono wa pande zote wa Saudi Arabia kwa kufanya mashauriano na viongozi wa Riyadh. Njia ya kutumia mabavu na ukandamizaji dhidi ya raia wa Bahrain ndio wenzo uliopendekezwa na Marekani na Saudi Arabia kwa watawala wa Manama katika kipindi hiki cha sasa. Kwani katika siku za hivi karibuni, utawala wa Aal Khalifa umezidisha vitendo vya mabavu na ukandamizaji dhidi ya wananchi wa Bahrain khususan wanawake. Hata hivyo mashambulizi ya vikosi vya Bahrain na Saudi Arabia dhidi ya wanawake wanaoandamana wa Bahrain na vilevile hatua ya vikosi hivyo ya kuzichoma moto nyumba na hata misikitiki ya ibada katika siku chache zilizopita, sambamba na safari iliyozusha maswali mengi ya Sheikh Hamad huko Saudia, kiujumla yote hayo yanadhihirisha namna utawala wa Bahrain ulivyokata tamaa. Ni wazi kuwa kama si misaada ya kijeshi na uungaji mkono wa majeshi ya Saudia na nchi nyingine za Kiarabu za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi na vilevile uungaji mkono wa Marekani kwa watawala wa Manama, basi utawala wa Aal Khalifa usingeweza kukabiliana hadi hivi sasa na wimbi kubwa la mapinduzi ya nchi nzima ya wananchi wa Bahrain.