IQNA

Wanaolalamikia siasa za kikandamizi za Saudia kuhukumiwa kama magaidi

8:31 - October 10, 2011
Habari ID: 2201941
Utawala wa Saudi Arabia umesema kuwa utawachukulia kuwa magaidi, wananchi wa nchi hiyo wanaolalamikia siasa za kiukandamizaji za utawala huo, zinazowahukumu raia katika mahakama za kijeshi.
Utawala huo umesema kuwa utawahukumu kama magaidi watu waliohusika katika ghasia za hivi karibuni katika maeneo yenye wakazi wengi wa Kishia mashariki mwa nchi hiyo na hasa mji wa Awamiya.
Hakimu mmoja wa mahakama za Saudia amesema kuwa watu waliotiwa nguvuni katika ghasia hizo hawatahukumiwa kama raia wa kawaida bali watahukumiwa kama magaidi wa mtandao wa al-Qaida.
Akifafanua zaidi suala hilo Hakimu Abdallah al Atim wa Mahakama ya Rufaa ya Saudi Arabia amesema kuwa watuhumiwa wa vitendo vya ghasia hizo watafikishwa mahakamani hivi karibuni na kuhukumiwa kama magaidi wanaohatarisha usalama wa Saudia mara tu baada ya kumalizika uchunguzi dhidi yao. Hakimu huyo amedai kwamba vitendo vya watuhumiwa hao vinafanana na vya magaidi kwa sababu amesema vinazusha woga na hofu kwenye jamii, vinaashiria nia ya wahusika kuasi amri ya walii wao na kwamba wamevuruga usalama wa nchi.
Baadhi ya maafisa wa ngazi za juu katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudia walidai hivi karibuni kwamba baadhi ya watu waliowatuhumu kuwa wanataka kujitenga mashariki mwa nchi hiyo waliwafyatulia risasi askari usalama katika matukio ya hivi karibuni na kujeruhi kadhaa kati yao. Walidai pia kwamba nchi moja ya kigeni, wakikusudia Iran, ndiyo inayowachochea wakazi hao ambao wanadhulumiwa na kukandamizwa kwa miaka mingi na utawala wa nchi hiyo. 876024

captcha