Kwa mujibu wa IQNA, kikao hicho kilifanyika Mei 20 kuhudhuriwa na Ayatullah Mojtahed Shabestari Imamu wa Sala ya Ijumaa Tabriz ambaye pia ni mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mkoa wa Azerbaijan, Meya wa Tabriz Alireza Novin, Alireza Zojaji Mkuu wa Masuala ya Utamaduni Katika Shirika la Jihadi ya Vyuo Vikuu, Hujjatul Islam wal Muslimin Sayyed Mahdi Taghavi, Mkuu wa Shughuli za Qur'ani za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu Iran na maafisa wengine wa mkoa huo.
Meya wa Tabriz ameelezea furaha yao kuwa mji huo ni mwenyeji wa mashindano ya Qurani na kuongeza kuwa mashindano hayo yatafanyika Septemba 12-15 ambapo maqari na mahufadh kutoka zaidi ya nchi 50 duniani watashiriki.
Hujjatul Islam wal Muslimin Sayyed Mahdi Taghavi amesema mialiko 83 imetumiwa kupitia idara za utamaduni za Iran katika nchi za kigeni na kuongeza kuwa wanaharakati wa Qur’ani katika vyuo vikuu mbali mbali duniani wameonyesha raghba ya kushiriki katika mashindano haya.
Kwa upande wake Ayatullah Mojtahed Shabestari Imamu wa Sala ya Ijumaa mjini Tabriz amesema mashindano hayo ni fursa nzuri ya kukabiliana na propaganda chafu za Mawahhabi dhidi ya Uislamu na madhehebu ya Shia. Mwanazuoni huyo amesema Qur’ani Tukufu ina nafasi muhimu katika kuwaongoza vijana na kuharakisha wimbi la mwamko wa Kiislamu duniani. Aidha amesisitiza umuhimu wa kuwahimiza Waislamu na hasa wanafunzi wa vyuo vikuu na vijana kujifunza kuhusu Qur’ani Tukufu.
1013004