IQNA

Sheikh Taruti: Washiriki wote wa ‘Dawlat al-Tilawa’ nchini Misri ni washindi kupitia Tajiriba

21:28 - September 16, 2025
Habari ID: 3481241
IQNA – Sheikh Abdel Fattah Taruti, qari mashuhuri wa Misri na mjumbe wa majopo ya majaji wa mashindano ya Qur’ani ya “Dawlat al-Tilawa”, amesema kwamba kila mshiriki katika mashindano hayo ni mshindi, hata ikiwa hatofika katika hatua ya mwisho.

Mashindano ya “Dawlat al-Tilawa” ni miongoni mwa mashindano makubwa zaidi ya usomaji wa Qur’ani yanayopeperushwa moja kwa moja kupitia televisheni nchini Misri. Yanaandaliwa na Wizara ya Awqaf (Wakfu) kwa ushirikiano na kampuni ya United Media Services, kwa lengo la kugundua na kukuza vipaji vipya vya usomaji wa Qur’ani Tukufu.

Akizungumza na kituo cha televisheni Youm7 mwishoni mwa raundi ya pili, Sheikh Tarouti alisema kwamba kitendo cha kushiriki pekee ni ushindi. “Kila mshiriki katika hatua hii tayari ameshinda kwa kupata tajiriba na hata kama hatofuzu kuingia fainali,” alisema.

Akaongeza kuwa mashindano ya mwaka huu yamevutia idadi kubwa ya washiriki. “Tumeshuhudia sauti zenye nguvu na zenye matumaini makubwa. Hii ni mara ya kwanza katika miaka ya karibuni kuona idadi kubwa ya washindani kama hivi, na wote wanastahiki kuungwa mkono,” alibainisha.

Sheikh Taruti pia aliisifu Wizara ya Awqaf kwa kuweka mazingira ya kweli ya mafunzo na hamasa kwa vijana wenye vipaji. Alisema hatua hiyo itasaidia kulea kizazi kipya cha wasomaji wa Qur’ani watakaorithi turathi ya wasomaji mashuhuri wa Misri.

Akasema kuwa washiriki bora wanapaswa kuchaguliwa kwa umakini mkubwa. “Siku moja, washindi hawa watasoma Qur’ani katika radio za Misri. Haipendezi msomaji aliyebobea kufanya makosa, hata kama ni madogo,” alionya. Pia alieleza matarajio yake binafsi kuhusu raundi ya mwisho, akiwatakia washiriki wote mafanikio.

Mashindano haya yanakusudia kuibua sauti mpya zinazofuata njia ya wasomaji wakubwa wa Misri kama vile Sheikh Abdul Basit Abdus Samad, Sheikh Mohammed Siddiq al-Minshawi, na Sheikh Mustafa Ismail. Aidha, yanalenga kuimarisha nafasi ya Misri kikanda na kimataifa katika kuendeleza turathi ya Qur’ani.

Zaidi ya washiriki 4,000 walisajili kushiriki. Mashindano ya awali ya kitaifa yaliyofanyika kati ya tarehe 6–11 Septemba 2025 yalihusisha washiriki 300. Washiriki 28 waliobakia watafanyiwa mafunzo ya kiutendaji mbele ya kamera mnamo tarehe 25 Septemba, na hatua ya mwisho imepangwa kufanyika Oktoba 2025.

3494620

captcha