IQNA

Kongamano la kimataifa la chapa ya Qur'ani kufanyika Madina

18:55 - June 11, 2012
Habari ID: 2344548
Kongamano la kimataifa la uchapishaji Qur'ani Tukufu limepangwa kufanyika hivi karibuni katika mji mtakatifu wa Madina nchini Saudi Arabia.
Kongamano hilo litafanyika kwa ushirikiano wa Jumuiya ya Uchapishaji Qur'ani ya Madina na Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kiislamu ya Saudia. Wanazuoni, wanafikra na wasomi wa Kiislamu ambao ni wataalamu katika masuala ya uchapishaji na usambazaji Qur'ani na vilevile wawakilishi wa serikali na mashirika ya sekta binafsi yanayojishughulisha na masuala ya Qur'ani kutoka nchi mbalimbali yamealikwa kushiriki katika kongamano hilo. Swaleh Aali Sheikh, Waziri wa Wakfu na Masuala ya Kiislamu wa Saudi Arabia ambaye pia ndiye msimamizi wa jumuiya iliyotajwa ya uchapishaji Qur'ani mjini Madina amesema kuna makala mengi ya kiutafiti yatakayowasilishwa katika kongamano hilo kuhusiana na uchapishaji Qur'ani. Amesema makala yatakayowasilishwa kwenye semina hiyo yatagawanywa kwa washiriki wa kongamano hilo. Historia ya chapa ya Qur'ani, mtazamo wa kielimu wa Qur'ani, mbinu za chapa na usambazaji Qur'ani, mada zinazotumika katika kuhifadhi Qur'ani pamoja na teknolojia ya chapa na usambazaji Qur'ani Tukufu ni miongoni mwa masuala muhimu yatakayojadiliwa katika kongamano hilo ambalo tarehe ya kufanyika kwake haijaainishwa. 1027212
captcha