Akiwahutubia wajumbe wa baraza kuu la Basiji (jeshi la kujitolea la wananachi) na wawakilishi wa matabaka mbalimbali ya mabasiji siku ya Alkhamisi mjini Tehran, Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei amesema kuwa, harakati za mabasiji hazina mipaka wala ukomo na kusisitiza kwamba mabasiji wako pia katika nyanja za ulinzi, ujenzi wa taifa, siasa, uchumi, sanaa, elimu na teknolojia na katika harakati za kidini. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, leo hii harakati na fikra za kujitolea za mabasiji zinashuhudiwa katika nchi za Iraq, Syria, Lebanon na Ghaza na kubainisha kwamba, fikra hizo zitaendelea kushuhudiwa huko Quds Tukufu kwa lengo la kuikomboa Masjidul Aqswa. Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina mushkeli wowote na wananchi wa Marekani na kusisitiza kwamba, taifa na wananchi wa Iran kamwe hawatasalimu amri mbele ya ubeberu wa Wamarekani. Ayatullah Khamenei amesifu juhudi kubwa zinazofanywa na timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kusema kuwa, kwa hakika ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo hayo na kundi la 5+1 umesimama imara katika kukabiliana na mabeberu, kinyume na ilivyo upande wa pili na hasa Marekani, kwani imekuwa ikibadilisha misimamo yake siku baada ya siku. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, iwapo mazungumzo hayo hayatafikia natija ya mwisho, Marekani ndiyo itakuwa mwathirika mkubwa na hasa ikizingatiwa kwamba, nchi hiyo hivi sasa inakabiliwa na matatizo mengi ya ndani na mpasuko mkubwa kati ya wananchi na serikali. Ayatullah Khamenei ameelezea matamshi yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa Marekani nje ya mazungumzo ya nyuklia ya kulindwa usalama wa utawala wa Israel na kusisitiza kwamba, makubaliano ya nyuklia yafikiwe au yasifikiwe Israel itazidi kukosa amani siku baada ya siku licha ya ukweli kwamba wanachojali viongozi wa Marekani ni maslahi yao na si usalama wa Israel. Ayatullahil Udhma Khamenei amesema kuwa, lengo kuu la Marekani ni kuuridhisha mtandao wa kimataifa wa wawekezaji wa Kizayuni, kwani mtandao huo hutoa rushwa na fedha kwa viongozi wa Washington; na kama viongozi wa nchi hiyo watajaribu kupinga matakwa yao, watakabiliwa na vitisho, kashfa na hata kutishiwa kifo.../mh