IQNA

Sifa za kipekee za jamii na serikali ya Kiislamu ya Mtume Muhammad SAW

20:57 - December 20, 2014
Habari ID: 2623557
Tumo katika kumbukumbu ya kufariki dunia Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu Muhammad al-Mustafa SAW. Hii leo imepita zaidi ya miaka 1400 tangu mbora huyo wa viumbe aage dunia; lakini jina la mtukufu huyo pamoja na utajo na shakhsia yake kubwa na adhimu na isiyo na mithili ingali inaleta hamasa katika nyoyo.

Zaidi ya Waislamu bilioni moja na nusu katika pembe mbalimbali duniani hushahadia risala ya Muhammad SAW katika Sala. Humswalia na kumtumia salamu na kufuata mafundisho yake. Kwa hakika msingi wa da’awa na ulinganiaji wa Mtume SAW ulisimama juu ya mafundisho ya Wahyi na Ufunuo; na ni kwa msingi wa mafundisho haya ndipo akaasisi na kuanzisha jamii na serikali ya Kiislamu ambayo imekuwa kigezo na ruwaza kwa dahari  na zama zote. Kigezo na sifa muhimu na ya kimsingi kabisa katika jamii na utawala wa Kiislamu ulioasisiwa na Bwana Mtume SAW kilikuwa ni kumpwekesha Mwenyezi Mungu, imani na umaanawi. Wito na nara ya Mtume SAW ya : قولوا لااله الا الله تُفلِحوا

“Semeni! Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu, ili mpate kufaulu” ilipelekea Mola Muumba afanywe kuwa mhimili na msingi muhimu katika maisha ya mwanadamu. Kwa msingi huo Mtume akawa ameleta mfumo wenye thamani kubwa na wa kubakia ambao umesimama juu ya msingi wa tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu.

Katika mfumo huo wa Tawhidi, mwanadamu kumuabudu mwanadamu mwenzake, kuabudu viumbe wengine au dunia kulizuiwa na kukatazwa. Ibada na uja ni makhsusi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kimsingi ni kuwa, falsafa ya kubaathiwa na kutumwa Mitume ilikuwa ni kwa ajili ya kuwafanya watu wamzingatie Mwenyezi Mungu na kujiepusha na aina yoyote ile ya utaghuti. Katika jamii ya Tawhidi iliyoundwa na Mtume SAW msukumo na injini ya harakati ilikuwa ni mapenzi na imani juu ya Mwenyezi Mungu. Imani ambayo ilikuwa ikifukuta katika nyoyo za watu na kuwapeleka watu kuelekea upande ulio sahihi.

Sifa na kigezo kingine katika jamii ya zama za Bwana Mtume SAW, ni kuzingatia mizizi ya elimu na maarifa. Umuhimu huu unaonekana wazi kwa kuzingatia aya ya kwanza aliyoshushiwa Bwana Mtume SAW ambayo ilikuwa ikikokoteza juu ya kusoma. Katika ustaarabu ambao Bwana Mtume SAW aliuasisi, vigezo vya watu katika jamii vilikuwa ni elimu na maarifa. Qur'ani Tukufu pia imewataja watu wenye elimu na maarifa kwamba, wana daraja kando ya watu wanaoshikamana na Taqwa na uchaji Mungu, wanaopigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wanaoshikamana na imani juu ya Mwenyezi Mungu.

Kimsingi ni kuwa, moja ya sababu za kubakia na kuenea utamaduni, ustaarabu na mifumo ya kisiasa na kijamii na kuoana kwake na elimu na maarifa. Ushahidi wa kihistoria na wa kuaminika unaonyesha kuwa, baadhi ya upotofu ambao ulikuwa hauoani na elimu na akili ulipelekea kuwekwa kando dini kama za Kikristo na Kiyahudi.

Kwa hakika miamala isiyo ya kiakili ya Kanisa ndiyo iliyoandaa mazingira mwafaka ya kukua fikra za kisekulari katika ulimwengu wa Magharibi. Lakini katika mfumo wa kijamii na ustaarabu wenye kubakia aliouleta Mtume SAW kwa ajili ya jamii ya wanadamu wa zama zote, kunashuhudiwa kwamba, mfumo wa Kiislamu sio tu kwamba, haukinzani na maendeleo ya kielimu na akili, bali daima unamshajiisha mwanadamu huyu kutafuta elimu, kutumia akili na kutafakari. Ni kutokana na utendaji huu ndio maana Uislamu ukawa kitovu na chimbuko la wanafikra na wasomi wakubwa katika taaluma mbalimbali ulimwenguni.

Sifa nyingine muhimu katika mfumo na dola ya Kiislamu ya Mtume ilikuwa ni kuzingatia na kulipa umuhimu suala la uadilifu. Uadilifu ni miongoni mwa mambo ya lazima na ya dharura katika ulimwengu, na sheria na kanuni za Mwenyezi Mungu zimewekwa kwa msingi huo. Bila ya kufanyiwa kazi uadilifu wa kijamii, mwanadamu hawezi kufikia katika saada, na bila ya uadilifu, jamii za wanadamu na nguvu za kisiasa duniani haziwezi kudumu na kubakia.

Mtume SAW alikuwa akiamiani kwamba, lengo kuu la kuasisi utawala wa Kiislamu ni kusimamisha uadilifu na usawa. Qur'ani Tukufu pia inatilia mkazo msingi wa uadilifu na daima inawataka na kuwashajiisha watu watekeleze uadilifu katika nyuga na nyanja mbalimbali. Katika zama zake na katika jamii ya Kiislamu na utawala wa Kiislamu aliouasisi, Mtume SAW alifanya idili ya kutekeleza uadilifu na insafu. Katika zama hizo za Mtume, watu wote walikuwa sawa katika jamii ya Kiislamu na hakuna mtu ambaye alikuwa mbora au aliye juu ya mwenzake isipokuwa kwa taqwa na uchaji Mungu.

Sifa nyingine ya mfumo wa kisiasa na kiutawala wa Mtume SAW ni umoja wa umma wa Kislamu. Ili kufikia lengo hilo, mbora huyo wa viumbe alifanya hima na idili kubwa. Hii leo makusudio ya umoja wa umma wa Kiislamu ni haya kwamba, Waislamu kila mmoja akiwa na madhehebu yake wajumuike pamoja katika mambo ya kidini yanayowakutanisha pamoja kama Tawhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, Qur’ani Tukufu, Mtume SAW, sunna na sira ya Mtume SAW mkabala na hatari zinazoikabili misingi na nguzo za Uislamu na jamii ya Waislamu. Kwa muktadha huo, Waislamu wanapaswa kushikamana, kuunganisha nyoyo zao na kujiweka mbali na tofauti za kimadhehebu, kisiasa, kikaumu na kilugha.

Moja ya mambo ambayo tunaweza kuyaashiria kama ni mbinu na mkakati muhimu wa Mtume wa Allah kwa ajili ya kuleta umoja ni namna alivyokuwa akiamiliana na watu sambamba na kujipamba kwake na tabia njema. Tabia njema, upole na ulaini wa Mtume SAW uliwavutia wengi na kuwa sababu muhimu ya kuzima hitilafu na mifarakano. Tabia yake njema wakati mwingine iliwafanya hata maadui wake wakubwa kuungana na wafuasi wake. Kwa msingi huo basi, tabia njema na ya kuvutia ya Mtume ilikuwa mhimili wa huba na kuzileta pamoja nyoyo za watu. Kutokana na Mtume SAW kufahamu na kudiriki vyema mazingira ya kijamii yaliyokuwa yakitawala katika zama hizo, aliandaa mazingira ya kuleta umoja baina ya watu.

Kuingia Madina Bwana Mtume SAW kulikwenda sambamba na kutiliana saini mikataba na makundi mbalimbali. Mikataba hiyo ilikuwa mikakati ya wazi kabisa kwa ajili ya umoja wa Kiislamu katika jamii ya wakati huo. Baada ya kuingia Yathrib, yaani Madina, Mtume Mtukufu alitayarisha mazingira ya kujenga umoja na mshikamano katika jamii mpya ya Kiislamu. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na mtukufu huyo ni kutayarisha mkataba wa kwanza kabisa katika Uislamu katika miezi ya mwanzoni mwa kuwepo kwake Yathrib (Madina). Mtume wa Mwenyezi Mungu aliandika mkataba kati ya Muhajirina na Ansar. Mkakati mwingine uliotumiwa na Bwana Mtume SAW ili kuhakikisha umoja wa umma wa Kiislamu unapatikana ni kupinga ukaumu, ukabila na ubaguzi. Uislamu ulipambana vikali na taasubi za kikaumu pamoja na ubaguzi na ukaweka bayana kwamba, kigezo cha ubora wa mtu sio rangi, kabila, taifa au utajiri bali ni taqwa na uchaji Mungu.

Tunatoa mkono wa pole kwa Waislamu na wapenda haki kote ulimwenguni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyoaga dunia na kurejea kwa Mola wake, mbora wa viumbe Mtukufu Mtume Muhammad SAW.

2623163

captcha