IQNA

Boko Haram wahujumu msikiti Nigeria, 26 wauawa

12:18 - May 31, 2015
Habari ID: 3309578
Waislamu 26 wamepoteza maisha baada ya magaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram kulipua bomu ndani ya msikiti mmoja katika mji wa Maiduguri kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Hujuma hiyo ya Jumamosi imejiri siku moja tu baada ya Muhammadu Buhari kutawazwa kama rais wa Nigeria ambapo ameapa kuangamiza kundi hilo la kigaidi sambamba na kuanzisha makao makuu mapya ya jeshi katika mji huo wa Maiduguri.
Katika tukio hilo la jana, gaini aliyekuwa amejifunga mshipi wa bomu alijilipua ndani ya Msikiti wa Alhaji Haruna kabla ya sala ya alasiri. Mkuu wa polisi katika jimbo la Borno Aderemi Padokum amesema nakala kadhaa za Qur'ani zimeteketea moto katika hujuma hiyo ya Boko Haram.
Katika taarifa Rais Buhari amelaani hujuma hiyo na kuapa kuchukua hatua dhidi ya magaidi.
Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Nigeria ya Kihausa  lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Zaidi ya watu elfu 13 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009. Boko Haram ni kundi lenye misimamo ya kufurutu mipaka nchini Nigeria ambalo kutokana na kuwa na ufahamu mbaya na potofu kuhusiana na Uislamu, limeitumbukiza nchi hiyo katika dimbwi la machafuko na mauaji sambamba na kuzusha hitilafu za kidini na kikabila nchini humo.../mh

3309515

captcha