Rais Rouhani ameyasema hayo leo mjini Tehran alipokutana na Mohammad Jihad al-Laham Spika wa Bunge la Syria ambapo amelipongeza pia taifa na serikali ya Syria kwa kusimama kidete na kupambana kishupavu. Rais Rouhani ameelezea matumaini yake kuwa, mapambano na jihadi ya wananchi na jeshi la Syria hatimaye itapelekea kupatikana ushindi dhidi ya magaidi. Aidha amesema Iran itaendelea kuiunga mkono Syria hadi mwisho. Rais Rouhani amesema hivi sasa Syria inakabiliana na vita vya kulazimishwa kutoka kwa baadhi ya nchi na makundi ya kigaidi. Ameongeza kuwa, wakati wa miaka ya kujihami kutakatifu, pamoja na kuwa dikteta wa Iraq Saddam alipata uungaji mkono wa nchi nyingi, taifa la Iran liliweza kupata ushindi. Spika wa Bunge la Syria kwa upande wake amewasilisha salamu maalumu za Rais wa Syria kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais, serikali na taifa la Iran. Amesema serikali na taifa la Syria kamwe halitasahau uungaji mkono wa nchi ndugu na rafiki ya Iran. Mohammad Jihad al-Laham amesema nchi za eneo zinazotekeleza hujuma dhidi ya Yemen na kuwaunga mkono magaidi Syria zinatekeleza mpango wa Marekani na madola mengine ya Magharibi na hakuna shaka kuwa hayo ni kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni wa Israel.../mh