Katika taarifa siku ya Ijumaa, Rupert Colville, msemaji wa Idara ya Kamishna wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa (OHCHR) ameashiria maombi ya mara kadhaa ya idara hiyo ya kutaka kuachiliwa mara moja Sheikh Salman, mwanachuoni wa Kishia ambaye pia ni mkuu wa chama cha upinzani cha al-Wefaq. Amesisitza kuwa, "Leo tunarudia tena wito huo." Sheikh Salman alitiwa mbaroni Desemba mwaka jana.
Colville ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya Sheikh Salman na mfungwa mwingine wa kisiasa Nablee Rajab ambaye ni mtetezi mashuhuri wa haki za binadamu. Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka ya kuendesha harakati dhidi ya utawala wa kidiktetea wa familia ya Aal Khalifa. Umoja wa Mataifa pia umeitaka Bahrain kusitisha ukandamizaji wa wapinzani nchini humo.
Maandamano ya wapinzani Bahrain yalianza mapema mwaka 2011 sambamba na mwamko wa Kiislamu katika eneo. Nchi hiyo ndogo katika Ghuba ya Uajemi ambayo ni muitifaki mkubwa wa Marekani na Uingereza katika eneo imekabiliana na waandamanaji kwa mkono wa chuma.../mh