Rais Rouhani amewatumia ujumbe viongozi wa nchi za Kiislamu duniani kwa mnasaba kuingia katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kusisitiza kuwa, ujumbe uliomo ndani ya mwezi huu ni rehema, amani udugu na urafiki. Rais wa Iran pia amesema ana matumaini kuwa, umoja, urafiki, mapenzi, amani na utulivu baina ya watu wa umma wa Kiislamu utaimarika zaidi ikilinganishwa na miaka iliyopita. Aidha katika ujumbe huo wa udugu na mapenzi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amevitaja vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na makundi yanayojinasibisha na Uislamu, mauaji ya watu wasio na hatia, ongezeko la ukatili na makundi yenye misimamo kufurutu ada, kuibua mifarakano na fitina baina ya Waislamu na kuuonyesha Uislamu kwa sura ya ukatili kunakofanywa na vyombo vya habari vya madola ya Magharibi, kuwa ni changamoto kubwa kwa ulimwengu wa leo wa Kiislamu. Amesema kuwa, kuna udharura kwa nchi za Kiislamu kushirikiana na kuimarisha umoja na udugu wa kidini baina yao zaidi ya kipindi kingine chochote kilichopita.
Wakati huo huoRais Hassan Rouhani wa Iran ameonya kuhusu kuenea harakati za magaidi Mashariki ya Kati na kwamba ugaidi haufaidishi nchi yoyote katika eneo hilo.
Rais Rouhani aliyasema hayo jana Alkhamisi katika mazungumzo ya simu na Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad bin Khalifa Al Thani. Rais Rouhani amesema 'nchi zote za eneo hili zinapata madhara kutokana na ugaidi hivyo vitendo vya kigaidi havifaidishi nchi yoyote na ni kizingiti katika ustawi na uhusiano bora baina ya nchi mbalimbali.' Rais Rouhani amesema kuna haja ya ushirikiano wa kieneo ili kurejesha amani na kwamba nchi za eneo hilo zinapaswa kuungana ili kukomesha umwagikaji damu katika mataifa ya Kiislamu. Rais wa Iran pia ametaka kuwepo mkakati wa kuwafikishia misaada ya dharura watu walioathiriwa vibaya na vita nchini Yemen.
Kwa upande wake mtawala wa Qatar ameutaja uhusiano wa Iran na Qatar kuwa wa kina, kihistoria na wenye nguzo imara na kwamba kuna haja ya kuboresha uhusiano huo. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaweza kuwa na nafasi muhimu katika kurejesha amani Mashariki ya Kati.../mh