Akihutubu siku ya Jumapili, kiongozi huyo wa harakati ya Ansarullah amesisitiza kuwa wananchi wa Yemen mwishowe watashinda kwa sababu wanakabiliwa na dhulma na wanapigana vita kwa ajili ya kutaka kujitawala. Abdul-Malik al-Houthi ameongeza kuwa mchokozi na mvamizi anaweza kupata mafanikio ambayo si ya kudumu na kwamba kile kitakachobakia ni uthabiti na uimara wa wananchi wa taifa la Yemen.
Abdul-Malik al-Houthi amesema adui Msaudi amepata mafanikio ya muda mfupi katika mji wa Aden na sasa anaeneza propaganda ili kufidia hasara kubwa aliyopata.
Kiongozi wa Ansarullah amesema Saudi Arabia, chini ya himaya ya Marekani, inatekeelza mauaji ya umati dhidi ya Watu wa Yemen. Amesema Wayemen hawatasalimu amri mbele ya matakwa ya watawala wa Saudia ambao wanataka kuiweka nchi hiyo chini ya satwa yao.
Saudi Arabia imekuwa ikitekeleza hujuma ya kinyama dhidi ya Yemen tokea Machi 26 ambapo zaidi ya watu 5,300 wameuawa wengi wao wakiwa ni raia hasa wanawake na watoto. Aidha jeshi la Saudia limehujumu na kubomoa nyumba za raia, misikiti, vyuo vikuu, shule, mahospitali,
viwanda na madaraja…/mh