Dkt. Helbawi ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Kiislamu Uingereza ameipongeza hatua hiyo ya Al Azhar kuitisha mkutano wa maulamaa wa Kishia na Kisuni.
Huku akiashiria mapatano ya nyuklia ya Iran yaliyofikiwa hivi karibuni huko Vienna baina ya Iran na madola sita makubwa duniani, Dkt Helbawi amesema: “Eneo linapaswa kufahamu mabadiliko yanayojiri na maana ya mapatano ya nyuklia baina ya Iran na nchi za Magharibi. Watu wa eneo hawapaswi kuitazama Iran kama adui hatari zaidi ya Israel kwa sababu hii ni fikra iliyopitwa na wakati.”
Dkt. Helbawi ambaye ni raia wa Misri ameongeza kuwa: “Hatua ya Shekhe Mkuu wa Al Azhar kuitisha kikao cha wanazuoni wa Kishia na Kisuni kwa lengo la kujadili umoja na tatizo la misimamo mikali ya kidini ni harakati muhimu sana ambayo itazimamoto wa fitina kwani hivi sasa tunashuhudia tatizo la utakfiri na kutolewa fatwa zinazochocheza zaidi mapigano ya kimadhehebu na mauaji.”
Wito wa Sheikh wa al Azhar , Sheikh Ahmed el-Tayyeb ulitolewa tarehe 22 Julai kupitia televisheni ya taifa ya Misri. Sheikh wa al Azhar alisisitiza udharura wa umoja baina ya Waislamu wa Shia na Suni. Aidha aliwahimiza maulamaa wa Kisuni kutoa fatwa zinazoharamisha mauaji dhidi ya Waislamu wa Kishia. Sheikh Tayyeb pia aliwataka maulamaa wa Kishia kutoa fatwa kama hiyo inayoharamisha mauaji dhidi ya Waislamu wa Kisuni.../mh