IQNA

Bahrain yakosolewa kwa kupiga marufuku gazeti la al-Wasat

6:34 - August 11, 2015
Habari ID: 3341173
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu nchini Bahrain wamesema kupigwa marufuku gazeti pekee la kujitegemea la al-Wasat nchini humo ni ukiukaji wa uhuru wa kutoa maoni.

Katika taarifa yao waliyotoa  Ijumaa, wanaharakati hao wa kutetea haki za binadamu wamesema uamuzi wa utawala wa Bahrain wa kulifungia gazeti binafsi la al-Wasat unakinzana na uhuru wa itikadi na wa utoaji maoni na kusisitiza kwamba hatua hiyo ni mwendelezo wa sera za ukandamizaji za utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya wapinzani na wakosoaji na inapasa kulaaniwa. Bodi ya serikali inayosimamia masuala ya vyombo vya habari nchini Bahrain siku ya Alkhamisi ilitangaza kuwa hadi litakapotolewa tangazo jengine, imepiga marufuku kuchapishwa gazeti la al-Wasat kwa tuhuma eti za kuchafua uhusiano wa Ufalme wa Bahrain na nchi nyengine na kuchapisha taarifa dhidi ya umoja wa kitaifa wa nchi hiyo. Lakini kwa mtazamo wa wananchi wa Bahrain lengo la kufungiwa gazeti la al-Wasat ni kuzidisha ukandamizaji na kuizima sauti ya wapinzani. Tovuti ya “Kioo cha Bahrain”imeandika kuhusiana na suala hilo kuwa bodi ya serikali inayosimamia masuala ya vyombo vya habari vya Bahrain imetangaza kwamba kusimamishwa gazeti la al-Wasat kumetokana na uvunjaji sheria na kuendelea kuchapisha mambo yanayoleta mifarakano ndani ya jamii na kutaka kuvuruga uhusiano wa Bahrain na nchi nyenginezo. Hali ya kuwa kitambo nyuma serikali ya Bahrain iliwahi kutoa taarifa ya vitisho dhidi ya vyombo vya habari kwamba endapo vitachapisha mambo ya kupinga serikali na kuwachochea wananchi vitachukuliwa hatua za kisheria. Taarifa hiyo ya utawala wa Aal Khalifa ilisisitiza kwamba ikiwa magazeti ya nchi hiyo hayatotoa mashirikiano kwa serikali yanaweza kuchukuliwa hatua. Nabil Rajab, mkuu wa kituo cha kutetea haki za binadamu nchini Bahrain naye pia ametoa radiamali kuhusiana na kusimamishwa uchapishaji wa gazeti la a-Wasat na kueleza kwamba kupigwa marufuku gazeti hilo ni kupuuza uhuru wa maoni na ni hatua kuelekea kwenye mustakabali wa kiza. Aidha amesisitiza kuwa uchukuaji hatua za usalama hautokomesha mgogoro wa Bahrain na kwamba mgogoro huo unhaitaji utatuzi wa kisiasa ambao njia pekee ya kupatikana kwake ni maridhiano ya kitaifa yatakayowezesha kuwepo uadilifu, usawa na kuheshimiwa haki za binadamu. Katika mahojiano ya mwisho aliyofanyiwa na gazeti la al-Wasat kabla ya kusimamishwa gazeti hilo, Nabil Rajab alisisitiza pia juu ya ulazima wa kupatiwa wananchi uhuru wa kiraia, kuwepo uadilifu na usawa na kuboreshwa hali ya maisha na haki za binadamu nchini Bahrain. Wakati huohuo wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano kutangaza mshikamano wao na wenzao walioko kizuizini kwa sababu za kisiasa. Huku wakiwa wamebeba bendera za nchi yao na picha za wanaharakati wa kisiasa walioko korokoroni waandamanaji hao walilaani jinai za utawala wa Aal Khalifa dhidi ya raia na mzingiro kiliowekewa kisiwa cha Sitre. Tangu Februari 14 mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa mapambano ya amani ya wananchi dhidi ya utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa, ambapo wananchi hao wanataka wawe na uhuru, kuwepo na uadilifu, kuondolewe ubaguzi na kuanzishwe utawala wa kidemokrasia unaotokana na ridhaa yao wenyewe nchini humo…/

3340852

captcha