IQNA

Msomi wa Al-Azhar atambuliwa kama “Mtu wa Mwaka wa Qur’ani” Katika Tuzo ya Kimataifa ya Qur’ani Libya

13:02 - October 05, 2025
Habari ID: 3481331
IQNA – Profesa Abdul Karim Saleh, Mkuu wa Kamati ya Mapitio ya Qur’ani ya Al-Azhar, ametangazwa na kupewa heshima kama “Mtu wa Mwaka wa Qur’ani” katika Tuzo ya 13 ya Kimataifa ya Qur’ani ya Libya.

Saleh, ambaye pia anaongoza jopo la majaji katika Mashindano ya Kimataifa ya Qur’ani ya Port Said nchini Misri, alitambuliwa na kamati ya waandaaji wa tukio hilo kwa mchango wake mkubwa katika kuhudumia Qur’ani na kueneza elimu zake nchini Misri na katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.

Profesa huyo amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za heshima katika huduma ya Qur’ani Tukufu na elimu zake. Ni mhadhiri wa Tafsiri, Sayansi ya Qur’ani na Qiraa katika Kitivo cha Qur’ani Tukufu cha Chuo Kikuu cha Al-Azhar, na aliwahi kuwa mkuu wa Idara ya Tafsiri, Sayansi ya Qur’ani na Qiraa katika kitivo hicho.

Saleh ni miongoni mwa wasomi mashuhuri wanaoshiriki katika majopo ya majaji ya mashindano ya kimataifa ya Qur’ani nchini Misri na mataifa mengine, na amewakilisha Al-Azhar katika mashindano makubwa ya kimataifa yaliyofanyika Makkah, Dubai, Bahrain, Libya na Sudan.

Aidha, amesimamia tafiti nyingi za kitaaluma katika vyuo vikuu vya Misri na nchi nyingine za Kiarabu, na ni mjumbe wa kamati za utoaji wa leseni za qiraa pamoja na bodi ya wahariri ya majarida maalumu ya sayansi ya Qur’ani, hali inayomfanya kuwa miongoni mwa sura mashuhuri za kisasa katika uwanja huo.

Kwa mujibu wa Adel Musalhi, mwanaharakati wa vyombo vya habari kutoka Misri, mafanikio haya ni hatua kubwa kwa mashindano ya kimataifa ya Qur’ani ya Port Said na yanadhihirisha hadhi ya jopo la majaji wa mashindano hayo, ambalo linajumuisha wataalamu wa Qur’ani wenye maarifa na tajriba ya hali ya juu.

Alisisitiza kuwa uteuzi wa Abdul Karim Saleh unazidi kuimarisha hadhi ya kimataifa ya mashindano hayo.

Inafaa kutaja kuwa toleo la tisa la Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi na Kusoma Qur’ani la Port Said litafanyika kuanzia Januari 30 hadi Februari 2, 2026. Toleo hilo limepewa jina la qari maarufu wa Misri aliyefariki dunia, Sheikh Mahmoud Ali Al-Banna.

3494872

captcha