IQNA

Indhari ya UNCR kuhusu hali mbaya ya Waislamu Myanmar

14:02 - August 31, 2015
Habari ID: 3354581
Umoja wa Mataifa umetoa indhari kuhusu wimbi jipya la wakimbizi wa Myanmar na Bangladesh wanaoelekea katika eneo la Asia Mashariki na yamkini jambo hilo likaibua maafa ya kibinadamu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi UNHCR limetaka hatua za haraka zichukuliwe  kabla ya kuanza mvua kali za msimu sambamba na kuanza wimbi la  wakimbizi wapya kutoka Ghuba ya Bengal.
Mwaka huu kumeshuhudiwa wimbi jipya la wakimbizi Waislamu wa kabila la Rohingya wa Myanmar ambao wamekuwa wakikimbia dhulma na ukandamizaji katika nchi hiyo inayotawaliwa na Mabudha. Wakimbizi hao walikumbwa na matatizo mengi wakati wakikimbilia nchi jirani za Thailand, Indonesia na Malaysia.
Mamia ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa na maelfu ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Mabudha hao wamekuwa wakiungwa mkono na vyombo vya dola. Umoja wa Mataifa pia umetangaza kuwa Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao wanaunda asilimia 5 ya watu milioni 60 nchini Myanmar ni moja kati ya jamii zinazodhulumiwa zaidi duniani.../mh

3354225

captcha