IQNA

Moto katika Msikiti wa Minneapolis Marekani wazua hofu miongoni mwa Waislamu licha ya taarifa ya ‘Ajali’

17:45 - October 01, 2025
Habari ID: 3481310
IQNA – Tukio la moto katika Msikiti wa Kituo cha Kiislamu Alhikma, ulioko Mtaa wa 32 kusini mwa Minneapolis, limezua wasiwasi mkubwa miongoni mwa viongozi wa Kiislamu, ambao sasa wanatoa wito wa uchunguzi wa kina, licha ya mamlaka za zimamoto kusema kuwa tukio hilo lilikuwa la bahati mbaya.

Moto huo ulizuka Jumatatu jioni, katika jengo linalohifadhi msikiti pamoja na kituo cha kulelea watoto. Kikosi cha zimamoto kilifika saa 11:31 jioni na kuzima nguo na takataka zilizokuwa zikiteketea karibu na mlango wa chini kabla moto haujasambaa ndani. Hakuna majeruhi walioripotiwa, na jengo halikupata madhara.

Idara ya Zimamoto ya Minneapolis ilihitimisha Jumanne kuwa chanzo cha moto kilikuwa cha bahati mbaya, huenda kikihusiana na watu wasio na makazi waliokuwa wakitumia eneo la ngazi. Polisi waliongeza kuwa takataka na vifaa vya dawa za kulevya vimekuwa tatizo la mara kwa mara katika eneo hilo.

Hata hivyo, viongozi wa jamii walihoji namna tukio hilo lilivyoshughulikiwa. Jaylani Hussein, mkurugenzi wa tawi la Minnesota la Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR), alisema kuwa maafisa hawakuwahoji mashahidi wala kuangalia kamera za usalama usiku wa tukio.

Alihimiza vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka, akionya kuwa “huenda kuna mshambuliaji mwingine bado yuko huru na anaweza kuanzisha moto mwingine.”

Jamii za Kiislamu katika Minnesota zimekumbwa na msururu wa mashambulizi dhidi ya misikiti katika miaka ya hivi karibuni. Hussein alisema kuwa walirekodi matukio 16 ya aina hiyo mwaka 2024 pekee. Mwezi uliopita, mtu mmoja alikiri kosa la kuchoma moto misikiti miwili katika miji ya Twin Cities mwaka jana.

Imamu wa Alhikma, Abdirizak Kaynan, alisisitiza kuwa kituo cha kulelea watoto kilichoambatana na msikiti huo huwa na watoto kati ya 50 hadi 60 kila siku, na akasema tukio hilo halikupaswa kuonekana tu “kama moto wa takataka katika kiwanja kisicho na watu.”

Polisi wamesema kuwa uchunguzi bado unaendelea na wanashirikiana na viongozi wa msikiti kupata picha za kamera za usalama. Msemaji wa polisi alisema: “Tunachukulia kwa uzito wasiwasi wa kila mwanajamii,” na kuwataka wote wenye taarifa kuwasiliana na wachunguzi.

3494827

Habari zinazohusiana
Kishikizo: marekani msikiti cair
captcha