IQNA

Lengo la Mashindano ya Qur'ani ya ‘Zayin al-Aswat’ latajwa

18:33 - October 01, 2025
Habari ID: 3481314
IQNA – Mkurugenzi mtendaji wa toleo la kwanza la mashindano ya Qur'ani ya kitaifa ya ‘Zayin al-Aswat’ (mapambo ya sauti) amesema kuwa katika mashindano mengi ya Qur'an, kila kitu huisha kwa sherehe ya kufunga na kuwatuza washindi na sasa sekretarieti ya tukio hili la Qur'an inalenga kuandamana na washiriki kupitia mawasiliano endelevu na yenye tija ili kuwafikisha katika viwango vya kitaalamu na vya kimataifa.

Toleo la kwanza la mashindano haya linafanyika mjini Qom leo na kesho (Oktoba 1–2) katika makundi matatu makuu chini ya kauli mbiu: “Qur'ani, Kitabu cha Waumini.”

Mohammad Reza Pourmoin, mkurugenzi mtendaji wa mashindano haya, aliambia Shirika la Habari za Qur'ani la Kimataifa (IQNA),: “Kuwepo kwa mashindano ya Qur'an na utofauti tunaouona ndani yake ni ishara ya uhai na msisimko wa jamii ya Qur'an nchini Iran. Na ukweli kuwa toleo hili la kwanza linatarajiwa kupokelewa kwa shauku kubwa ni ushahidi kuwa bado tunahitaji kuandaa matukio kama haya, hasa mashindano ya Qur'ani.”

Aliendelea: “Katika kuanzisha wimbi jipya la shughuli za Qur'ani, ni lazima tutafute mawazo mapya na mitazamo mipya. Matukio haya yanapaswa kubuniwa na kutekelezwa kwa namna inayokamilisha mashindano ya Qur'ani yaliyopo.”

Mtaalamu huyo mkongwe wa Qur'an aliongeza: “Inaonekana kuwa Zayen al-Aswat itafuata njia ya matukio mengine ya Qur'ani, lakini pia inalenga kuziba mapengo na masuala yaliyopuuzwa ambayo tumeyaona katika mashindano ya Qur'ani hadi sasa.”

Miongoni mwa masuala yaliyopuuzwa ambayo mashindano haya yanataka kushughulikia ni mawasiliano ya baada ya mashindano kati ya kamati ya maandalizi na washiriki, hasa washindi. Mara nyingi, sherehe ya kufunga na kuwatuza washindi haifuatwi na hatua nyingine. Isipokuwa kwa matukio machache yanayohusiana na juhudi binafsi za wasomaji au wahifadhi wa Qur'ani, hakuna muundo wa kisera au kiutendaji unaojitolea kuendeleza mafanikio ya washiriki.”

Alisisitiza kuwa Zayen al-Aswat inalenga kutimiza hilo kwa kukamilisha mzunguko wa mafunzo, kutambua vipaji vya vijana na vijana wadogo, na kuwajumuisha katika jamii za kitaalamu na za kimataifa za Qur'ani.

"Huenda swali likazuka kuwa miundo mingine iliwahi kubuniwa kwa mtazamo kama huu lakini haikufikia malengo yake kutokana na ukosefu wa vipengele muhimu kama ufadhili wa kifedha. Kwa hivyo, ni bora taasisi na mashirika ya Qur'ani yaungane na kuunganisha uwezo wao wa kitaalamu na kiufundi ili kuunda harakati imara na ya pamoja katika uwanja wa shughuli za Qur'ani, ikiwemo mashindano.”

Katika sehemu nyingine ya mazungumzo yake, Pourmoin alitaja uwepo wa wasomi na wataalamu wa Qur'ani wenye uzoefu mkubwa katika kamati ya kiufundi na ya majaji ya mashindano ya Zayen al-Aswat, akisema: “Hili, pamoja na sifa za kimfumo na za maudhui za mashindano haya, linaonyesha umuhimu wa nafasi ya mashindano haya katika kutambua na kukuza vipaji vipya vya usomaji wa Qur'an. Kwa hakika, kwa maendeleo na kuimarika kwa vipaji hivyo, masuala yote ya kisera na utekelezaji yatakabidhiwa kwao.”

3494833

captcha