IQNA

Maldives Yaripoti Ukuaji wa Kuhifadhi Qur'an, Idadi ya Ma-Hafidh Yaongezeka

17:49 - October 01, 2025
Habari ID: 3481311
IQNA – Serikali ya Maldives (Maldivi) imetangaza kuwa sasa kuna zaidi ya watu 280 waliothibitishwa kama ma-Hafidh wa Qur'an, huku wengine zaidi ya 1,500 wakiendelea na programu za kuhifadhi Qur'an, kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Katika ujumbe kwa vyombo vya habari vya ndani, wizara hiyo ilisema kuwa watu 284 katika taifa hilo la visiwa wamekamilisha kuhifadhi Qur'ani kwa ukamilifu. Wengi wao walipata mafunzo katika Kituo cha Qur'ani kinachoendeshwa na serikali pamoja na taasisi nyingine za kidini.

Waziri wa Mambo ya Kiislamu, Mohamed Shaheem Ali Saeed, alibainisha kuwa ma-Hafidh wengine 50 wanatarajiwa kuhitimu wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Aidha, alithibitisha kuwa Rais Mohamed Muizzu atatoa tuzo na medali kwa ma-Hafidh hao usiku wa 27 wa Ramadhani, usiku unaoheshimiwa sana katika tamaduni za Kiislamu.

Serikali hivi karibuni imeongeza posho ya kila mwezi kwa ma-Hafidh kutoka Rufiyaa 2,000 (takriban dola 130 za Kimarekani) hadi Rufiyaa 4,000, na malipo hayo tayari yameanza kutolewa.

Maldives ni taifa dogo la visiwa katika Bahari ya Hindi lenye watu takriban nusu milioni, ambapo karibu wote ni Waislamu. Kuhifadhi Qur'an ni sehemu muhimu ya elimu ya dini nchini humo, na taasisi za serikali zinaunga mkono mafunzo na kutambua mafanikio ya wale wanaokamilisha safari hiyo ya kiroho.

3494824

 

captcha