Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, tovuti ya hqmi.org imeripoti kuwa mashindano hayo ya kuhifadhi Qur'ani yamefanyika kwa ushirikiano baina ya Jumuiya ya Vijana Waislamu Zimbabwe na Jumuiya ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur'ani Tukufu ambapo kulikuwa na washiriki 30 wa kiume na kike. Mashindano hayo yalikuwa katika kategoria tatu za kuhifadhi Juzuu 15, Juzuu 10 na Juzuu 5 ambapo kulikuwa na majaji sita katika mashindano hayo. Aidha sherehe za kuwaenzi waliopata nafasi za juu katika mashindano hayo zilifanyika katika Msikiti wa Arcadia mjini Harare na kuhudhuriwa na Sheikh Adam Salam Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Zimbabwe, Sheikh Moustafa Bhatia wa Baraza Kuu la Waislamu Zimbabwe, mwakilishi wa Jumuiya ya Awn ya Kuwait na Hani Mohamad Ar Ramadi mwakilishi wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur'ani miongoni mwa shakhsia wengine wa Kiislamu na waalimu wa Qur'ani. Waliozungumza katika hafla hiyo walitoa wito wa kufanyika jitihada zaidi katika uga wa kuhifadhi na tajwidi ya Qur'ani Tukufu.../mh