Maafisa wa Saudi Arabia wanaohusika na matukio ya maafa wameripoti kuwa tukio hilo lilijiri leo huko Mina saa tatu asubuhi kwa wakati wa huko, baada ya makundi mawili makubwa ya mahujaji waliokuwa wakitokea katika mitaa ya 204 na 223 kukutana pamoja na hivyo kusababisha msongamano na kukanyagana kwa mahujaji. Ajali hiyo imetokea wakati mahujaji walipokuwa wakielekea kutekeleza amali ya hija ya kumpiga mawe shetani mlaaniwa. Wakati huo huo Sa'eed Ohadi Mkuu wa Taasisi ya Hija ya Iran amesema kuwa Wairani 90 ni miongoni mwa mahujaji walioaga dunia katika msongamano huo huko Mina na kwamba wengine 150 wamejeruhiwa. Amesema katika siku ya kwanza ya kutekeleza amali ya Jamarat ambapo mahujaji kutoka nchi zote huelekea huko Mina kutekelezea amali hiyo, ilitangazwa kuwa, njia mbili zimefungwa na kwamba mahujaji wataweza kuelekea Mina kwa kutumia njia tatu tu. Amesema tukio hilo chungu na la kushtua limetokea kwa sababu hiyo na kwa kuzingatia idadi kubwa na msongamano wa mahujaji.../mh