"Suleiman Bello aliamua kumuogopa Allah kwa kudiriki kuwa atasimama mbele yake siku ya Qiyama," amesema Abdullahi Mohammed mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Hija Nigeria (NAHCON).
"Aliamua kuwa balozi mzuri wa Nigeria. Aliokota mfuko na kuupelekea kwa wasimamizi wa msafara wake wa hija na kisha tukaurejesha kwa mmiliki wake. Jambo hili linaonyesha Wanigeria ni watu waaminifu na wenye kumuogopa Mwenyezi Mungu."
Mwislamu huyo Mnigeria, Suleiman Bello, alienda Hija mwaka huu kama sehemu ya msafara wa Hija kutoka jimbo la Nasarawa la kati mwa Nigeria.
Belo aliuokota mfuko huo karibu karibu na Ka'aba ndani ya Msikiti Mkuu wa Maka na kukabidhi mfuko huo wa Tume ya Kitaifa ya Hija Nigeria. Mbali na US$ 2,345 mfuko huo ulikuwa pia na 3,020 fedha za Kiafghani. Mmiliki wa mfuko huo, Mosa Gousdin, alijulikana kutokana na vitambulisho vilivyopatikana ndani yake. Gousdin amemshukuru kwa dhati Bello kwa uaminifu wake.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe wa Afghanistan, Sayed Tahir Hashimi alisema hana maneno ya kutosha ya kumshukuru raia huyo wa Nigeria. Kwa kuzingatia kitendo hicho cha uaminifu, Tume ya Kitaifa ya Hija Nigeria imemtuuku zawadi Bello ikiwemo tiketi ya kushiriki katika ibada ya Hija mwakani.