Katika mahojiano ya Televisheni siku ya Alhamisi, Sayyid Hassan Nasrallah amelaani mashambulizi ya Saudi Arabia huko Yemen yanayofanyika eti kwa lengo la kumrejesha madarakani rais aliyetoroka nchi na kusema, jamii ya kimataifa haipasi kukaa kimya mbele ya jinai za utawala wa kifalme wa Saudia nchini Yemen. Ameongeza kuwa mapambano na kusimama kidete kwa taifa la Yemen katika kipindi cha miezi saba iliyopita kumethibitisha kwamba, Wayemeni wamechagua njia yao na hawatasalimu amri kwa Wasaudia.
Katika sehemu nyingine ya matamshi yake Katibu Mkuu wa Hizbullah amezungumzia nafasi ya Syria na uungaji mkono wa serikali ya Damascus kwa wanamapambano wa Lebanon na Palestina na akasema, suala la kuiangamiza Syria limekuwa katika ajenda ya siku zote ya Marekani. Sayyid Nasrallah amesisitiza kuwa hadi sasa mabilioni ya dola yametumika kuiangamiza Syria, mamia ya tani za silaha yametumika kuua watu wa nchi hiyo na maelfu ya magaidi kutoka pembe mbalimbali za dunia wamekusanywa na kupelekwa Syria kutimiza malengo ya Marekani na waitifaki wake huku vyombo vya habari vya Kiarabu na Kimataifa vikiendesha propaganda chafu na kueneza uchochezi wa kidini na kimadhehebu kwa lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Damascus. Amesema njama hizo zimefeli kutokana na mapambano ya Wasyria na msaada wa nchi zinazopinga ubeberu kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.