Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, Washiriki wa kongamano hilo wamelaani vitendo hivyo vya ugaidi na wamesisitizia umuhimu wa kuenezwa kwa utamaduni wa kuitafakari Qur'ani kwa ajili ya kuwaepusha vijana kujiunga na magenge hayo yanayotumia dini ya Kiislamu katika kutenda jinai. Zaidi ya wanafikra na wasomi wakubwa 500, kutoka nchi 30 za dunia, walishiriki kongamano hilo la pili la kimataifa katika mji wa Casablanca (Dar Al-Baïda) nchini Morocco. Kongamano hilo lililofanyika kwa kusimamiwa na taasisi ya kusimamia Qur'an, lilianza asubuhi ya Jumatano kwa kuhudhuriwa na shakhsia mbalimbali wa kielimu wakiwamo wahadhiri wa vyuo vikuu, wafanyatablighi na wataalamu wa masuala ya Qur'ani Tukufu kutoka nchi tofauti za Kiarabu na Kiislamu.
Mwishoni mwa kongamano hilo washiriki hao wametoa taarifa ya pamoja wakisisitizia juu ya udharura wa kufungamana na Qur'an kitabu hicho cha mbinguni sanjari na kuwaonya vijana kunako kuhadaiwa na watu wanaojinasibisha na Uislamu na kutenda jinai dhidi ya binaadamu kote duniani.
Aidha washiriki walitoa wito wa kuanzishwa mbinu mpya za kueneza mafundisho ya Qur’ani tukufu hasa kwa kutumia teknolojia za kisasa za habari na mawasiliano.