Rais Rouhani alisema hayo leo mbele ya Baraza lake la Mawaziri na sambamba na kuienzi tarehe 4 Novemba, ambayo nchini Iran inajulikana kwa jina la Siku ya Taifa ya Kupambana na Mabeberu Duniani amesisitiza kuwa: Wananchi wote wa Iran ni kitu kimoja katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na katika kulinda uhuru na kusimama kidete mbele ya mabeberu. Amesema, nasaha na maagizo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu yanalenga kwenye kutia nguvu uwezo wa kitaifa wa Iran ili taifa la Iran liweze kuwa kitu kimoja na kusimama safu moja katika kupambana na njama za madola baki yanayojaribu kujipenyeza kiuadui humu nchini. Amesema, wananchi wa Iran wanaijua vyema maana ya kujipenyeza mabeberu katika mambo yao na wanavitambua vyema vitendo visivyo sahihi vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Rais Rouhani ameongeza kuwa, vijana, mabarobaro, wanachuo na wanafunzi wa Iran wamethibitisha kuwa wote wako kwenye safu moja ya Mapinduzi ya Kiislamu na wamethibitisha pia kuwa, mapinduzi hayo matukufu hayahusiana na watu wa rika fulani tu.