IQNA

Afrika Kusini yamfukuza Kaimu Balozi wa Israel

17:22 - January 31, 2026
Habari ID: 3481876
IQNA –Afrika Kusini imemtangaza kaimu balozi wa utawala wa Isarel nchini humo kuwa mtu asiyehitajika na kuamuru afukuzwe mara moja.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imetangaza kuwa nchi hiyo inamfukuza mjumbe huyo wa Israel aliyekuwa akihudumu nchini humo, kutoka na kujihusisha na kile ilichokitaja kuwa ni “ukiukwaji usiokubalika wa misingi na kanuni za diplomasia,” vitendo ambavyo, kwa mujibu wa wizara hiyo, vinadhoofisha mamlaka ya Afrika Kusini kama taifa huru.

Hatua hiyo imekuja katika mazingira ya mvutano unaozidi kuongezeka kati ya Pretoria na Tel Aviv, huku Afrika Kusini ikisisitiza dhamira yake ya kulinda heshima ya taifa, misingi ya diplomasia ya kimataifa, na uhusiano unaojengwa kwa kuheshimiana.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini ambayo rasmi inajulikana kama Idara ya Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano (DIRCO) ilisema Ijumaa kuwa imempa Ariel Seidman, kaimu balozi (chargé d’affaires) katika ubalozi wa Israel, muda wa saa 72 kuondoka Afrika Kusini baada ya kumtangaza kuwa persona non grata yaani mtu asiyehitajika.

Idara hiyo ilimtuhumu Seidman kwa kufanya “mashambulizi ya matusi” dhidi ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa kupitia mitandao ya kijamii, pamoja na kile ilichokitaja kuwa ni “kushindwa kwa makusudi” kuijulisha wizara hiyo kuhusu “ziara za maafisa waandamizi wa Israel” nchini humo.

“Vitendo kama hivyo ni matumizi mabaya makubwa ya haki na fursa za kidiplomasia, na ni ukiukaji wa msingi wa Mkataba wa Vienna.

“Tunalihimiza Serikali ya Israel kuhakikisha kuwa mwenendo wake wa baadaye wa kidiplomasia unaonyesha heshima kwa Jamhuri ya Afrika Kusini na kanuni zilizokubaliwa za mahusiano ya kimataifa,” iliongeza taarifa hiyo.

Tangazo hilo lilizua majibu ya haraka kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, ambayo ilisema kuwa nayo imemtangaza kumtimua mwanadiplomasia mwandamizi wa Afrika Kusini, Shaun Edward Byneveldt,  na kumpa muda wa saa 72 kuondoka katika utawala wa 'Israel'.

Kwa mujibu wa tovuti ya serikali ya Afrika Kusini, Shaun Edward Byneveldt ni balozi wa Afrika Kusini katika Dola ya Palestina, akifanya kazi kutoka ofisi iliyopo Ramallah katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Chrispin Phiri, alisema kuwa “vizingiti na ubishi wa Israel vimeilazimisha hali ya kuchekesha ambapo [Byneveldt] analazimika kuidhinishwa kupitia utawala ule unaokalia kwa mabavu nchi anayowakilisha.”

“Jambo hili linaonyesha wazi msimamo wa Israel wa kukataa kuheshimu muafaka wa kimataifa kuhusu taifa la Palestina,” Phiri aliandika kupitia mtandao wa X.

Kesi ya Mauaji ya Kimbari

Hatua hizi za kulipizana kisasi kidiplomasia zimekuja wakati mvutano kati ya Afrika Kusini na Israel ukiendelea kuongezeka kwa miezi kadhaa, kufuatia vita vya mauaji ya kimbari vya Isarel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Mwisho wa Desemba 2023, Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ikiituhumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari katika eneo hilo linaloshambuliwa vikali.

“Afrika Kusini ina wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya raia waliokwama katika mashambulizi ya sasa ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, kutokana na matumizi ya nguvu bila ubaguzi na uhamishaji wa watu kwa lazima,” nchi hiyo ilisema wakati huo.

Taarifa hizi zimeendelea kuashiria mwelekeo wa msimamo imara wa Pretoria katika kutetea haki za Wapalestina na kuheshimu misingi ya haki za kimataifa, kwa mujibu wa maelekezo ya jumuiya ya kimataifa.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika makubwa ya haki za binadamu duniani pia wameituhumu Israel kwa kutekeleza mauaji ya kimbari huko Gaza, ambako mashambulizi ya Israel yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 71,660 tangu Oktoba 2023 na kusukuma eneo hilo katika mgogoro mkubwa wa kibinadamu.

Wanaharakati wa Afrika Kusini nao wamezua ghadhabu ya maafisa wa Israel kwa kuutuhumu utawala huo kuwa unaendesha mfumo wa ubaguzi wa rangi (apartheid) katika jinsi inavyowatendea Wapalestina , mfumo unaofanana na ule uliokuwapo Afrika Kusini kwa miongo kadhaa.

Habari inayohusiana:

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema mapema mwezi huu kuwa Israel inaendesha “aina kali sana ya ubaguzi wa rangi na utengaji wa watu unaofanana na mfumo wa apartheid ambao tumeshuhudia hapo awali.”

Ijumaa, chama cha upinzani cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini kiliikaribisha hatua ya serikali ya kumtimua kaimu balozi wa Israel.

“Kuanzia ukiukwaji wa mara kwa mara wa maazimio ya Umoja wa Mataifa, hadi kukaidi wazi mahakama za kimataifa, pamoja na mashambulizi ya wazi dhidi ya wanadiplomasia, waandishi wa habari, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na raia huko Palestina na kwingineko, Israel imejijengea taswira ya utawala wa kihuni unaotegemea vitisho na uchokozi badala ya heshima ya pande zote,” chama hicho kilisema katika taarifa yake.

EFF pia kiliitaka Afrika Kusini “kuendelea kuchukua misimamo thabiti na ya kimaadili dhidi ya Israel ya kibaguzi,” ikiwemo kukata kabisa mahusiano yote ya kidiplomasia na kiuchumi na nchi hiyo.

3496247

Habari zinazohusiana
captcha