IQNA

Wimbi jipya la chuki dhidi ya Uislamu baada ya hujuma za Paris

12:18 - November 15, 2015
Habari ID: 3451758
Kiongozi mmoja anayejihusisha na harakati za kusimamia haki za Waislamu na wahajiri waishio katika viunga vya jiji la Paris, Ufaransa ameonya juu ya kushadidi wimbi kubwa la chuki dhidi ya Waislamu kutokana na mashambulizi ya kigaidi nchini humo.

Nazer Kaha, mwanaharakati wa haki za binaadamu na kutatua matatizo ya Waislamu na wahajiri mjini Paris, amesema kuwa baada ya mashambulizi ya kigaidi hapo juzi, basi Waislamu wajiandae kushuhudia wimbi la chuki na vitendo vya maudhi dhidi yao. Sanjari na kulaani hujuma hiyo, amesisitiza kuwa kwa kawaida kila kunapotokea vitendo kama hivyo hujiri wimbi la ubaguzi na chuki dhidi ya Waislamu ambao nao hawahusiki hata kidogo na ugaidi huo. Mwanaharakati huyo ametaka umoja baina ya Wafaransa wote na kutekelezwa juhudi za makusudi kwa ajili ya kuzuia aina yoyote ya migogoro inayoweza kuibuka kufuatia hujuma hiyo ya juzi ya kigaidi. Hii ni katika hali ambayo Rais François Hollande wa Ufaransa ametangaza hali ya hatari na siku tatu za maombolezo kufuatia mashambulizi hayo ya kigaidi yaliyotekelezwa katika maeneo tofauti ya jiji la Paris na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS auDaesh nchini humo. Watu zaidi ya 130 wamethibitishwa kuuawa na zaidi ya 200 kujeruhiwa katika jinai hiyo inayoenda kinyume na ubinaadamu na dini Tukufu ya Kiislamu.

3447863

captcha