Kamati hiyo ya haki za binadamu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa imepanga kuwasilisha rasimu ya azimio kwenye baraza hilo kuhusiana na suala hilo. Ijapokuwa maazimio ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hayana ulazima wa utekelezaji lakini yana taathira kubwa katika uchukuaji maamuzi. Waislamu wa jamii ya Rohingya ambao idadi yao ni milioni moja na laki tatu ni sehemu ya jamii ya watu zaidi ya milioni 50 wa Myanmar. Kwa mujibu wa ripoti, wagombea kadhaa Waislamu walinyimwa fursa ya kugombea ubunge katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni nchini Myanmar kwa kisingizio kwamba hawana uraia wa nchi hiyo. Ripoti hiyo aidha inaonyesha kuwa mamia ya maelfu ya Waislamu wa Myanmar walinyimwa haki ya kupiga kura katika uchaguzi huo. Uchaguzi wa kwanza huru nchini Myanmar baada ya miaka 26 ya utawala wa kijeshi ulifanyika tarehe 8 ya mwezi huu wa Novemba. Mamia ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wameuawa na maelfu ya wengine kulazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi ya kikatili yanayofanywa na Mabudha wenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu. Umoja wa Mataifa pia umetangaza kuwa Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar ni moja kati ya jamii zinazodhulumiwa zaidi duniani.