Katika ripoti yenye anuani ya "Watoto wetu wanadondoshewa mabomu", Amnesty imekosoa namna ndege za kivita za Saudia zilivodondosha mabaomu katika shule za mikoa ya Sana'a, Hajjah na Hudaydah magharibi mwa Yemen kati ya Agosti na Septemba. Amnesty imesema hakuna ushahidi wowote uliopatikana kuwa shule hizo zinatumika kijeshi na kuongeza kuwa watoto 6,500 wamevurugiwa masomo katika mikoa hiyo. Aidha shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema Marekani na Uingereza ni washirika katika jinai hizo za kivita za Saudia kwani madola hayo makubwa ya magharibi ni wauzaji wakuu wa silaha zinazotumiwa na Saudia na waitifaki wake kuwaua watoto wa Yemen.
Mapema mwezi Oktoba Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa ulitoa taarifa na kusema zaidi ya watoto 500 Yemen wameuawa katika hujuma za Saudia. Saudi Arabia na waitifaki wake tarehe 26 Machi mwaka huu walianzisha mashambulizi dhidi ya wananchi wa Yemen ili kuiondoa madarakani Harakati ya Ansarullah na kuirejesha madarakani serikali iliyojiuzulu. Raia zaidi ya 7,600 wameuawa, wengi wakiwa ni raia wa kawaida hasa wanawake, watoto na wazee huku wengine wengi wakilazimika kuwa wakimbizi kutokana na mashambulizi hayo huku miundo mbinu ya nchi hiyo kama vile mahospitali, shule na misikiti ikiharibiwa vibaya. Wakati huo huo harakati ya Ansarullah imetangaza kuafiki pendekezo la Umoja wa Mataifa kuhusu usitishwaji vita Yemen. Msemaji wa Ansarullah Mohammed Abdulsalam amesema wameafiki usitishwaji vita, kuondolewa mzingiro na kuanzishwa mazungumzo ya kisiasa. Saudi Arabia kwa muda mrefu imekuw apingamizi la usitishwaji vita nchini Yemen.