Katika taarifa ya mwisho ya kikao hicho, washiriki kutoka maeneo yote ya dunia wameonya kuhusu hatari ya njama ya kuangamziwa baadhi ya nchi za Kiislamu hasa Syria, Iraq na Yemen na kusema njama hizo ni kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni na madola ya kibeberu na kiistikbari duniani. Washiriki aidha wametoa wito wa kufanyika jitihada maradufu ili kurejesha amani na usalama katika eneo na kuzuia kugawanyika vipande vipande nchi zinazolengwa. Washiriki pia wamekosoa vikali wale wanaochochea fitina za kimadhehebu na kikabila mambo ambayo yanapelekea kuvunjiwa heshima matukufu ya Waislamu. Aidha washiriki wameashiria matukio ya hivi karibuni ya mauaji na ukandamizaji wa Waislamu huko Nigeria na Jamhuri ya Azerbaijan ambapo wamelaani yaliyojiri katika nchi hizo. Wameitaka serikali ya Nigeria iwachukulie hatua waliohusika na fitina na mauaji ya mamia ya Waislamu sambamba na kuainisha hatima ya mwanazuoni mwanamapambano Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye pia ni mwanachama wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madehebu za Kiislamu.
Mkutano huo wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu pia umesisitiza kuwa kadhia ya Palestina ingali inasalia kuwa kadhia muhimu zaidi katika Ulimwengu wa Kiislamu na kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel ndio chanzo cha matatizo na migogoro katika ulimwengu wa Kiislamu.
Halikadhalika washiriki wa kikao hicho cha Tehran wamesema maamuzi muhimu duniani yanapaswa kuchukuliwa pasina kuwepo mashinikizo ya utawala wa Kizayuni na madola ya kibebebru na kiistikbari. Katika taarifa hiyo ya mwisho, washiriki wamesisitiza kuwa uwezo na utajiri mkubwa wa Ulimwengu wa Kiislamu utumike kwa ajili ya maendeleo na ustawi na kuangamiza umasikini katika nchi za Kiislamu. Kongamano hilo pia limesisitiza kuhusu ulazima wa kushirikiana vyuo vikuu vya nchi za Kiislamu ili kuhimiza utamaduni wa kukurubisha madhehebu sambamba na kuarifisha Uislamu halisi ambao unapingania na misimamo mikali pamoja na utumiaji mabavu.
Katika sherehe za kufunga mkutano huo wa umoja wa Kiislamu hapa Tehran pia walienziwa wanazuoni ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kukurubisha madhehebu za Kiislamu. Mkutano wa 29 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulimalizika Jumanne usiku baada ya kuendelea kwa muda wa siku tatu ambapo kulikuwa na washiriki 600 kutoka nchi 70 za maeneo yote ya dunia.