Vyombo vya habari vya Uingereza vimeripoti kuwa mvulana Mwislamu mwenye
umri wa miaka 10 aliandika katika somo lake la lugha ya Kiingereza kuwa anaishi
katika "terrorist house" yaani nyumba ya gaidi lakini kusudio lake
lilikuwa ni "terraced house" ibara inayotumiwa Uingereza kumaanisha mlolongo
wa nyumba.
Baada ya kuona kosa la mvulana huyo, shule iliwasiliana na polisi kutokana na sheria inayoshurutisha shule zote kutoa ripoti kuhusu chochote kinachoweza kuwa na uhusiano na misimamo mikali.
Polisi ya Kaunti ya Lancashire imetoa taarifa na kusema afisa wa polisi na mfanyakazi wa huduma za jamii walimtembelea mvulana huyo nyumbani kwao katika eneo mji mdogo wa Accrington kufuatia kosa hilo la tahajia.
Baada ya hapo polisi walisema: "Hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi na hivyo hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa."
Familia hiyo sasa inataka msamaha kutoka kwa polisi na shule kwa sababu mtoto huyo amebughudhiwa kisaikolojia. "Hivi sasa ana hofu ya kuandika kwa kutumia ubunifu wake," binamu yake amewaambia waandishi habari. Jina la mvulana huyo halijatangazwa. Akizungumza na gazeti la Telegraph, baba ya mtoto huyo amesema: "Alirejea nyumbani kutoka shuleni akiwa mgonjwa. Kisha polisi wakaja hapa na kunifahamisha kuwa shule imesema amejihusisha na kitendo cha kigaidi. Polisi hawakua na adhabu. Walichukua laptop. Kwa hakika nimeshtushwa na tabia ya polisi. Wamamchukulia hatua mtoto wangu kwa sababu tu ni Mwislamu." Ameongeza kuwa familia yake ni ya Kiislamu na haina uhusiano wowote na ugaidi.
Tokea kulipojiri hujuma za kundi la kigaidi la ISIS au Daesh mwezi Novemba mwaka jana ambapo watu zaidi ya 130 waliuawa, kumeshuhudiwa kuongezeka vitendo vya chuki dhidi ya Waislamu kote Ulaya hasa nchini Uingereza na Ufaransa.
Kuna takriban Waislamu milioni 2.7 kati ya idadi ya watu milioni 53 nchini Uingereza.
Wiki hii Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amewataka wanawake wa Kiislamu ambao ni wahamiaji nchini humo kujifunza Kiingereza au watimuliwe.