
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya
Kiislamu aliyasema hayo Jumamosi jioni mjini Tehran alipoonana na Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya
Watu wa China na ujumbe alioandamana nao. Huku akigusia historia
kongwe ya uhusiano wa kibiashara na kiutamaduni baina ya mataifa mawili
ya Iran na China amesisitiza kuwa: Serikali na taifa la Iran muda wote
lilikuwa na linaendelea kufuatilia suala la kustawisha uhusiano wake na
nchi huru na zinazoaminika kama vile China na ni kwa sababu hiyo ndio
maana makubaliano baina ya marais wa Iran na China ya kuwa na uhusiano
wa kiistratijia wa miaka 25 yakawa ni makubaliano sahihi kabisa na ya
hekima sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja
matamshi ya Rais wa China kuhusiana na ulazima wa kufufuliwa na
kuhuishwa "Njia ya Hariri" na kustawishwa ushirikiano kati ya nchi
zilizoko kwenye njia hiyo kuwa ni fikra nzuri kikamilifu na ni fikra
inayokubalika na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe
haitoweza kusahau ushirikiano mzuri wa China katika kipindi cha vikwazo.
Ayatullah
Udhma Khamenei amelitaja suala la nishati kuwa moja ya masuala muhimu
katika dunia ya leo na kusisitiza kuwa: Iran ndiyo nchi pekee huru
katika eneo hili ambayo inaweza kuaminiwa katika upande wa nishati kwani
tofauti na baadhi ya nchi za eneo hili, siasa za Iran kuhusiana na
nishati haziathiriwi na kitu chochote kile kisichokuwa cha Kiirani.
Vile
vile ameashiria siasa za kibeberu za baadhi ya nchi hususan Marekani na
ushirikiano wao usio na mwamana na nchi nyingine na kuongeza kuwa:
Jambo hilo limezifanya nchi huru kupanua zaidi ushirikiano baina yao na
kwamba makubaliano ya Iran na China ya kuwa na uhusiano wa kiistratijia
wa miaka 25 yamefikiwa katika fremu hiyo hiyo na kwa hakika inabidi
pande mbili zilipe uzito mkubwa suala la kufuatilia makubaliano hayo na
kuyaingiza kwenye hatua za utekelezaji.
Kiongozi Muadhamu wa
Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna utamaduni wa Iran unavyopenda
na unavyovutika upande wa Mashariki na kuongeza kuwa: Wamagharibi
hawajahi kufanikiwa kuvutia imani ya taifa la Iran.
Ayatullah Udhma
Khamenei amesema kuwa, siasa za Marekani kuhusu Iran ni mbaya zaidi na
ni za kiuadui zaidi ikilinganishwa na za nchi nyingine za Magharibi na
kuongeza kwamba: Ni siasa hizo za kiuadui za Marekani ndizo
zilizolifanya taifa la Iran na viongozi wa nchi hii kulipa umuhimu suala
la kustawisha uhusiano wake na nchi huru duniani.
Vile vile
amesisitiza kuwa: Kuunga mkono suala la "China Moja" ni katika siasa za
kimsingi na zisizobadilika za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na amegusia
matamshi ya Rais wa China kuhusu kustawishwa na kuimarishwa uhusiano wa
kiusalama baina ya nchi mbili hizi na kuongeza kuwa: Ni jambo la
kusikitisha kuona kuwa eneo letu hili limekumbwa na ukosefu wa amani
kutokana na siasa ghalati za Wamagharibi na vile vile welewa mbaya,
potofu na ghalati kuhusu mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Amesema:
Kuna hatari hali hiyo ikawa mbaya zaidi hivyo inabidi kuwe na
ushirikiano wa kweli na wa busara ili kuzuia kutokea jambo kama hilo.
Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, baadhi ya nchi za eneo
hili ndizo chanzo kikuu cha fikra hizo potofu na kuongeza kuwa:
Wamagharibi nao, badala ya kupambana na chanzo cha fikra na makundi hayo
ya kigaidi, wanawashambulia na kuwashinikiza Waislamu barani Ulaya na
Marekani wakati makundi hayo ya kigaidi yanatofautiana kikamilifu na
fikra sahihi ya Uislamu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia namna
Wamarekani na Wamagharibi wanavyong'ang'ania kutumia jina la "dola la
Kiislamu" kuyaita baadhi ya makundi ya kigaidi na kusema: Kung'ang'ania
msimamo huo ni kuwavunjia heshima Waislamu na badala ya kutatua tatizo
lililopo, msimamo huo - kwa njia isiyo ya moja kwa moja - unaandaa
uwanja wa kuimarika na kuzidi kupata nguvu makundi hayo.
Aidha
ameyataja madai ya Wamarekani ya kudai kuunda muungano wa kupambana na
ugaidi kuwa ni hila tu za dola hilo la kibeberu na kusisitiza kuwa: Huo
ndio msimamo wa Wamarekani katika masuala yote na kamwe hawana mwamana
katika vitendo vyao vyote.
Mwishoni mwa matamshi yake, Kiongozi
Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea matumaini yake kwa kusema:
Matokeo ya mazungumzo na makubaliano ya Tehran yatakuwa na manufaa kwa
pande zote mbili kwa maana halisi ya neno.
Katika mazungumzo hayo
ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiisamu ya
Iran, Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China ameelezea
kufurahishwa kwake na kupata fursa ya kuitembelea Iran kama ambavyo
ameshuruku kwa mapokezi mazuri, ya kiudugu na kiikhlasi aliyoyapata
kutoka kwa serikali na taifa la Iran. Amesema mapenzi hayo yanatokana na
kuweko ushirikiano na mabadilishano ya kirafiki na ya muda mrefu baina
ya nchi mbili hizi na kuongeza kuwa: Ushirikiano wa pande mbili kati ya
Iran na China umesimama juu ya msingi wa kulinda manufaa ya pande hizo
na inabidi ushirikiano huo upanuliwe na kustawishwa zaidi kadiri siku
zinavyosonga mbele.
Rais wa China ameashiria historia ndefu ya
mawasiliano baina ya Iran na China kupitia njia ya kale ya kibiashara
maarufu kwa jina la "Njia ya Hariri" na kusema kuwa, njia hiyo ni nembo
ya amani, maendeleo na mabadilishano ya kiurafiki ya kibiashara.
Ameongeza kuwa: Nchi zilizoko kwenye njia hiyo, zinaweza kushirikiana
zaidi na kufikia malengo yao ya ustawi kupitia ushirikiano huo na
kujiwekea kinga nzuri mbele ya kigezo cha kiuchumi cha Wamarekani
kinacholenga kuvuruga milingano ya kiuchumi katika eneo hili.
Bw. Xi
Jinping amesema: Baadhi ya madola makubwa ya kibeberu yanataka kuhodhi
kila kitu na yanaendesha siasa za msituni za "imma uwe na sisi au uwe
adui yetu" lakini maendeleo ya uchumi unaochipukia hivi sasa
yameyapokonya madola hayo udhibiti wa uchumi duniani na yameandaa uwanja
mzuri kwa ajili ya kuimarika fikra na siasa za tawala huru ulimwenguni.
Rais wa China amelitaja suala la uungaji mkono wa nchi yake kwa
"kadhia ya nyuklia ya Iran" na pia uungaji mkono wa Iran kwa suala la
"China moja iliyoshikamana" kuwa ni mfano mzuri wa kuweko kuaminiana na
pia kuwa na siasa huru nchi hizi mbili na kuongeza kuwa: Sisi
tunaendelea kwa uhuru na njia yetu ya ustawi na tuko tayari - kama
tulivyokuwa pamoja na Iran katika kipindi chote cha vikwazo - kuendelea
kuwa pamoja na Iran na kupanua ushirikiano wetu katika nyuga zote baada
ya kuondolewa vikwazo.
Bw. Xi Jinping amegusia faida nyingi za
kijiografia, nguvu kazi na nishati za Iran na kusema: Uchumi wa China na
Iran unahitajiana na unakamilishana na katika ziara yangu hii tumefikia
makubaliano kuhusu mipango ya ushirikiano wa kiistratijia wa miaka 25
na tuko tayari kupanua na kuimarisha ushirikiano katika sekta nyingine
zote za kiutamaduni, kielimu, kiteknolojia, kijeshi, na kiusalama katika
kiwango cha washirika wa kiistratijia.
Rais wa China amesema, ni
jambo la dharura kuwa na mikakati mizuri ya kuongeza wigo wa ushirikiano
wa kiusalama baina ya nchi mbili katika kukabiliana na ugaidi na
masuala mengine tata kwenye eneo hili.
Aidha Bw. Xi Jinping amesema
kuwa, matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni ya
hekima sana na amemwambia Kiongozi Muadhamu kwamba: Serikali na taifa la
China linakuangalia kwa jicho la upendo, udugu na urafiki na ni
matumaini yetu utasaidia kustawi zaidi uhusiano wa nchi hizi mbili kama
ulivyofanya huko nyuma.
3469696