IQNA

Waislamu Mali kuishtaki Saudia kuhusu maafa ya Mina

17:14 - February 18, 2016
Habari ID: 3470146
Baadhi ya familia za Waislamu wa Mali waliopoteza maisha katika maafa ya Mina wakati wa Hija mwaka jana wameazimia kuushtaki utawala wa Saudia.

Hayo yamedokezwa na wakili wao, Marcel Ceccaldi ambaye amekosoa vikali utendaji wa Saudia wakati wa msongamano mkubwa wa watu wakati wa msimu wa Hija Septemba 26 mwaka 2015 karibu na mji mtakatifu wa Makka. Amesema familia za waathirika zimepanga kuwasilisha malalamiko dhidi ya ufalme wa Saudia nchini Mali na katika Umoja wa Ulaya.

Ceccaldi pia ameikosoa vikali serikali ya Mali kutokana na ilivyoshughulikia maafa hayo.

Saudi inadai kuwa ni watu 770 waliofariki katika maafa hayo lakini maafisa wa Shirika la Hija la Iran wanasema ni takribani Waislamu 4,700 waliopoteza maisha katika tukio hilo wakiwemo Wairani 465. Shirika la Habari la AFP linasema limerekodi watu 2,426 waliopoteza maisha katika maafa hayo.

Saudia imekosolewa vikali kutokana na usimamizi wake mbovu wa Hija na hasa maafa ya Mina ambayo yalijiri siku chache tu baada ya kuanguka winchi au kreni katika Msikiti Mtakatifu wa Makka ambapo watu zaidi ya 100 waliaga dunia na wengine 200 kujeruhiwa.

3459119


captcha