
Miripuko hiyo ilitokea Jumapili mkoa wa Damascus katika wilaya ya Sayeda Zeinab, katika barabara ya al-Tin karibu na Haram ya Bibi Zeinab SA, mjukuu wa Mtume Mtukufu SAW. Miripuko iliyotokea ni minne ikiwemo miwili ilioyolenga magari katika barabara ya al-Tin. Kundi la kigaidi na kitakfiri la ISIS ambalo limekuwa likifanya mashambulio ya aina hiyo nchini Syria na Iraq, limetangaza kuhusika na mashambulizi hayo ya kigaidi ambapo waliopoteza maisha ni raia wa kawaida. Miripuko hiyo imetokea masaa machache baada ya kutokea mashambulizi mengine mawili katika mkoa wa Homs, magharibi mwa Syria, ambapo watu zaidi 57 wameripotiwa kuuawa na wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa. Waziri Mkuu wa Syria Wael al-Halqi amelaani mashambulizi hayo dhidi ya raia wasio na hatia na kusisitiza kuwa, taifa la Syria litaendelea kusimama kidete kupambana na ugaidi. Hii ni katika hali ambayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia ametaka magaidi walioko nchini Syria waimarishwe kwa silaha. Adel al-Jubeir amesema hayo katika mahojiano aliyofanyiwa na gazeti la Kijerumani la Der Spiegel na kutamka waziwazi bila ya kificho kuwa makundi yanayobeba silaha (akikusudia magenge ya kigaidi) lazima yapatiwe makombora ya kutungulia ndege. Al-Jubeir ameongeza kijeuri kuwa, endapo magenge hayo yatakuwa na silaha za kisasa, yataweza kuipindua serikali ya Syria.