Ikumbukwe kuwa Desemba 12 mwaka jana, wanajeshi wa Nigeria waliwashambulia Waislamu waliokuwa katika kituo cha Kiislamu cha mji wa Zaria jimboni Kaduna, na kuwatuhumu kuwa walifunga njia ya msafara wa mkuu wa jeshi kwa njama ya kumuua.
Waislamu wa eneo hilo wamepinga vikali tuhuma hizo. Siku moja baadaye, jeshi la Nigeria lilivamia nyumba ya Sheikh Ibrahim Zakzaky na kumtia mbaroni sambamba na kuua mamia ya Waislamu waliokuwa wakimlinda. Katika matukio hayo mawili, mamia ya wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria waliuawa kwa umati, wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky. Baadhi ya duru zinadokeza kuwa waliouawa katika tukio hilo ni zaidi ya elfu moja.
Katika mahojiano maalumu na IQNA, Bi. Zakiya Zakzaky amesema baba yake na mama yake wangali wanashikiliwa katika hospitali moja ya vikosi vya usalama.
Ameongeza kuwa tokea Aprili Mosi, hakuna mtu yeyote aliyeruhusiwa kuwatembelea wazazi wake na hiyo hali yao ya kiafya haijulikano. Ameongeza kuwa Sheikh Zakzaky angali na risasi tumboni ambayo haiwezi kutolewa kutokana uwezekano wa maisha yake kuwa hatarini zaidi.
Akiashiria mauaji ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, mwezi Desemba, Bi.Zakiya Zakzaky alisema wanajeshi waliingia nyumba ya wazazi wake na kuanza kufyatua risasi pasina kufanya uchunguzi wowote. Anaongeza kuwa wanajeshi waliamuru wanawake wote kuvua Hijabu, jambo ambalo anasema ni ishara ya chuki dhidi ya Uislamu miongoni mwa wanajeshi hao wa Nigeria.
Anaongeza kuwa baada ya mauaji ndani ya nyumba ya Sheikh Zakzaky, katika ziku zilizofuata, jeshi lilifunga barabara zote zilizokuwa zinaelekea mjini humo na kupekea simu za mkononi au mobile za waliokuwa wakiingia mjini humo na kumuua papo hapo kila ambaye katika simu yake kulikuwa na picha za Sheikh Zakzaky au Imam Khomeini MA au Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Bi. Zakiya Zakzaky katika mahojiano yake na IQNA pia ameashiria vikao vya mahakama ambavyo vimefanyika baad aya mauaji ya Zaria na kusema mahakama hiyo ya Nigeria haitaku uadilifu wala haina nia ya wa kuwatia hatiani waliotekeleza mauaji ya Zaria.
Hivi karibuni, Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Kiislamu ya Uingereza imetangaza kuwa faili la mauaji ya Waislamu katika mji wa Zaria nchini Nigeria limewasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko The Hague nchini Uholanzi.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Haki za Binamu ya Kiislamu ya Uingereza (IHRC) Bwana Mas'ud Shajareh anasema kuwa ukubwa wa jinai hiyo na mwenendo wa serikali ya Nigeria wa kupuuza mauaji hayo vinalazimu kufanyika uchunguzi kuhusu mauaji ya mamia ya Waislamu katika mji wa Zaria.