IQNA

Sayyid Hassan Narallah

Marekani inataka kushadidisha machafuko Mashariki ya Kati

10:06 - October 13, 2016
Habari ID: 3470609
Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa Marekani ina mkono katika migogoro na machafuko yanayoendelea kushuhudiwa katika eneo la Mashariki ya Kati.
Aidha amewataka wananchi na viongozi wa mataifa ya eneo hili kuwa macho na njama za Washington na washirika wake za kushadidisha machafuko na migogoro hiyo.

Sayyid Hassan Narallah alitoa wito huo Jumanne katika maadhimisho ya Tasua na Ashura ya Imam Hussein (as) kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Alisema, baada ya Marekani kutia mkono wake katika migogoro ya Syria, Yemen na Iraq, kutokana na kushindwa njama zake huko Iraq, sasa inafanya juu chini kuingiza magaidi ndani ya ardhi ya Syria kutokea mji wa Mosul kaskazini mwa Iraq na kuwapeleka huko Deir Az Zor ili kuweza kuendeleza mgogoro nchini Syria.

Katibu Mkuu wa Hizbullah ameashiria kugonga mwamba mazungumzo ya amani ya Yemen na Syria na kueleza kwamba kutokana na uafriti na ukwamishaji wa Marekani hakuna mwanga wowote wa matumaini kuhusu hatima ya kisiasa ya migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati na kwamba kwa kuitumia vibaya hali iliyojitokeza, Marekani inafanya kila njia kuimarisha nafasi yake na waungaji mkono wake kwa kuwaingiza nchini Syria magaidi wa kundi la kitakfiri la Daesh kutokea kaskazini mwa Iraq.

Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ametoa sisitizo hilo la kuwa macho na hatua za kichochezi na chokochoko za Marekani na waungaji mkono wake wa eneo ikiwemo Saudi Arabia na Uturuki katika hali ambayo, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, Marekani imetoa kipaumbele kwa operesheni za kushambulia ngome za jeshi la Syria; Uturuki imerefusha uwepo wake kijeshi ndani ya ardhi ya Iraq; nayo Saudi Arabia imeua kwa halaiki mamia ya raia wa Yemen katika mji mkuu Sana'a katika shambulio la umwagaji damu mkubwa zaidi kuwahi kufanya katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita dhidi ya nchi hiyo.

Matukio na mabadiliko yanayojiri katika eneo kama alivyoeleza Katibu Mkuu wa Hizbullah yanaoneysha kuwa licha ya matatizo yote, muqawama wa kukabiliana njama za Washington ndio njia bora kabisa ya kuhakikisha haki za mataifa zinapatikana na kushindwa mipango ya kujipanua inayotekelezwa dhidi ya nchi za eneo hili.

3461146

captcha