IQNA

Indhari

Kiongozi wa Hizbullah: Utawala wa Israel 'utalipa kwa damu' mauaji ya raia wa Lebanon

9:53 - February 17, 2024
Habari ID: 3478364
IQNA-Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema utawala wa Israel "utalipa kwa damu" gharama ya mauaji ya hivi karibuni ya raia kusini mwa nchi hiyo, akisisitiza kwamba mauaji hayo hayawezi kuifanya harakati hiyo kuacha kuwaunga mkono Wapalestina katika Ukanda wa Gaza unaozingirwa.

Sayyed Hassan Nasrallah alisema hayo katika hotuba ya televisheni iliyotangazwa moja kwa moja kutoka mji mkuu wa Lebanon wa Beirut siku ya Ijumaa kwa mnasaba wa Siku ya Viongozi  wa Hizbullah Waliouawa Shahidi, ambayo huadhimishwa kila mwaka Februari 16.

Hotuba hiyo imekuja siku mbili baada ya utawala wa Israel kulenga jengo moja katika mji wa Nabatiyeh kusini mwa Lebanon, na kusababisha vifo vya watu saba wa familia moja akiwemo mtoto.

Katika shambulio jingine la utawala huo haramu, mwanamke mmoja na watoto wake wawili pia waliuawa katika kijiji cha as-Sawana kusini mwa Lebanon.

Nasrallah alilaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Nabatiyeh na as-Sawana kama "mauaji ya kimakusudi," na akasema Tel Aviv lazima ijue kwamba "ilikwenda mbali sana" kwa kuwalenga raia.

Akisisitiza kuwa lengo la utawala wa Israel la kuua raia ni kushinikiza kukomeshwa muqawama au mapambano, Nasrallah alisema: "Tuko katika kitovu cha vita vya kweli kwenye mstari ambao una urefu wa zaidi ya kilomita 100, na kuuawa shahidi wapiganaji wetu ni sehemu ya vita. ”

Kiongozi huyo wa Hizbullah alisema kulengwa hivi karibuni kwa kitongoji haramu cha walowezi wa Kizayuni cha Kiryat Shmona kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa makombora kadhaa ya Katyusha ni "jibu la awali" kwa umwagaji damu wa Jumatano, na kuongeza kuwa wanamapambano wa Lebanon wana uwezo mkubwa na sahihi wa makombora ambayo yanaweza kuenea kutoka Kiryat Shmona kaskazini hadi Eilat kusini.

Sayyid Hassan Nasrallah aidha amesema: "Licha ya kila kitu ambacho adui na Wazayuni wanafanya katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Gaza, Wamarekani na Waisraeli lazima waelewe kwamba huko Palestina wanakabiliwa na watu ambao hawatarudi nyuma.".

Nasrallah pia amewashukuru wanajeshi wa Yemen kwa kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya meli za Marekani na Uingereza katika Bahari ya Sham kwa ajili ya kuwaunga mkono Wapalestina na kusisitiza kuwa vita kuu ni Gaza.

Mkuu huyo wa Hizbullah aliikashifu Washington kwa uungaji mkono wake usioyumba kwa Israel katika vita vyake vya mauaji ya kimbari huko Gaza na kusema maafisa wa Marekani "wanawajibika hasa kwa kila tone la damu inayomwagika katika eneo hilo."

4200132

Habari zinazohusiana
captcha