IQNA

Amnesty yaitaka Bahrain imuachilie huru Sheikh Salman mara moja

19:09 - April 17, 2017
Habari ID: 3470937
TEHRAN (IQNA)-Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka Bahrain imuachilie huru mara moja mwanazuoni maarufu wa Kiislamu Sheikh Ali Salman.

Wito huo umetolewa Jumapili siku chache baada ya mahakama ya utawala wa Bahrain kuidhinisha kifungo cha miaka mitano cha Sheikh Salman ambaye pia ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Jumuiya ya Kitaifa ya Kiislamu ya Al Wefaq ambacho kimepigwa marufuku nchini humo.

Amnesty International imesisitiza ku,wa Sheikh Salman anapaswa kuachiliwa huru mara moja na bila masharti yoyote. Taasisi hiyo ya kimataifa pia imeutaka utawala wa ukoo wa Aal Khalifa nchini Bahrain kuheshimu uhuru wa maoni na kubatilisha sheria ambazo zinaharamisha hatua za amani. Amnesti inasema mahakama iliyosikiliza kesi ya Sheikh Salman haikuzungatia uadilifu na taratibu za kisheria.

Sheikh Salman,alitiwa nguvuni mwezi Desemba mwaka 2014 baada ya kutoa hotuba kadhaa za kupinga siasa za utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa katika mwamko wa Kiislamu unaoendelea katika nchi hiyo ndogo ya Ghuba ya Uajemi na ulioanza Februari 2011.

Wananchi wa Bahrain wamekuwa wakifanya maandamano makubwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo tangu mwaka 2011 wakitaka kuondoka madarakani utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa kufanyika uchaguzi huru na wa haki na kusitishwa ukandamizaji wa wapinzani.

3462604/
captcha