Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, hadi sasa zaidi wa sasa Waislamu 87,000 wa kabila la Rohingya wamepata hifadhi nchini Bangladesh kufuatia mauaji ya umati na ukatili dhidi ya nchini Myanmar. Katika kipindi cha wiki mbili sasa Waislamu wa Myanmar wanakabiliwa na wimbi jipya la hujuma za jeshi na Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu ada na hivyo wengi wamelazimika kukimbia kuokoa maisha yao.
Mji mdogo wa Ukhia nchini Bangladesh ni eneo lenye idadi kubwa ya wakimbizi Waislamu kutoka Myanmar na hapo wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Kutupalong ambayo ni kati ya kambi mbili za wakimbizi eneo hilo. Kambi nyingine inajulikana kama Nayapara. Kambi hizi mbili kwa ujumla zina wakimbizi takribani 30,000 wa jamii ya Rohingwa.
Hizo ni kati ya kambi za kwanza kabisa za ambazo zilipokea wimbi la kwanza la wakimbizi waliokimbia machafuko Myanmar mwaka 1992. Bangladesh yenyewe ambayo ni nchi ndogo lakini yenye idadi kubwa ya watu wanaokadiriwa kuwa milioni 162 ilikataa kuwasajili wakimbizi wapya Warohingya mwaka huo wa 1992. Lengo la sera hiyo lilikuwa ni kuwazuia Waislamu wa Rohingya kukimbilia nchini humo lakini kutokana na ukatili unaowakumba Waislamu hao hawana budi ili kukimbia nchi yao ya Myanmar inayotawaliwa na Mabuddha wenye misimamo mikali ya chuki dhidi ya Uislamu.
Pamoja na masaibu mengi wanayokumbana nayo, Waislamu katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh wanajitahidi kuwafunza watoto wao Qur’ani Tukufu na mafundisho mengine ya Uislamu. Watoto katika kambi hizo wanajifunza Qur’ani katika maeneo ya wazi au katika vyumba vidogo vyenye msongamano mkubwa.
Aidha Waislamu katika kambi hizo, pasina kuwepo msaada kutoka nje, wametumia udongo kujenga misikiti kwa ajili ya kutekeleza ibada zao za kila siku.
Waislamu katika maeneo mbali mbali duniani wanaendelea kulaani mauaji ya umati na ukatili wanaofanyiwa Waislamu nchini Myanmar lakini jamii ya kimataifa haijachukua hatua za maana kuzuia ukatili huo.