IQNA

Mkuu wa Al-Azhar: Machafuko na Kukosekana kwa Mantiki Duniani Yatokana na Kupuuzwa kwa Maadili ya Kidini

17:04 - November 03, 2025
Habari ID: 3481456
IQNA – Imamu Mkuu wa Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri, Sheikh Ahmad al-Tayyib, amesema kuwa dunia inakumbwa na machafuko na ukosefu wa mantiki, hali ambayo chanzo chake ni kupuuzwa kwa maadili ya kidini na kiutu.

Sheikh al-Tayyib aliyasema hayo Jumamosi katika makao makuu ya Al-Azhar mjini Cairo, alipokutana na Askofu Mkuu Edgar Peña Parra, Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Jumla wa Sekretarieti ya Vatican, akiwa ameandamana na Askofu Mkuu Nicholas Tavenin, Balozi wa Vatican nchini Misri.

Mwanzoni mwa kikao hicho, Askofu Peña Parra alifikisha salamu za Papa Leo wa XIV kwa Imamu Mkuu, akieleza matarajio yake ya kukutana naye na kumtakia afya njema na maisha marefu. Papa pia alieleza matumaini yake ya kuendeleza ushirikiano na Al-Azhar katika kueneza ujumbe wa amani na udugu kwa ulimwengu mzima.

Naibu Katibu Mkuu huyo alionesha furaha yake kukutana na Imamu Mkuu na kupongeza juhudi zake katika kuimarisha maadili ya amani ya kimataifa na udugu wa kibinadamu. Alisisitiza kuwa Hati ya Kihistoria ya Udugu wa Kibinadamu, iliyosainiwa na Sheikh al-Tayyib pamoja na Papa Francis (marehemu) huko Abu Dhabi, itaendelea kuwa kumbukumbu ya kudumu ya mshikamano wa kidini katika kueneza wema.

Alieleza kuwa mtazamo wa Sheikh al-Tayyib kuhusu hali ya dunia unalingana na ule wa Papa Leo XIV, na akasisitiza haja ya kuendeleza juhudi za pamoja kwa manufaa ya binadamu wote.

Kwa upande wake, Imamu Mkuu alithibitisha uhusiano wa kina kati ya Al-Azhar na Vatican, uhusiano uliodumu na kuimarika zaidi wakati wa uongozi wa Papa Francis. Alisema kuwa tangu walipokutana kwa mara ya kwanza, waliona mapenzi ya Papa kwa amani na kujitolea kwake kwa mazungumzo ya kidini—msimamo ambao pia umeendelezwa na Papa Leo XIV kupitia mawasiliano yao ya simu na misimamo yake kuhusu wanyonge, hasa katika Ukanda wa Gaza na Sudan.

Sheikh al-Tayyib alieleza matumaini yake ya kuendeleza ushirikiano kati ya Al-Azhar na Vatican katika kueneza ujumbe wa amani, udugu, na mazungumzo ya kidini kwa watu wote.

Kuhusu Changamoto za Kisasa

Imamu Mkuu alieleza kuwa dunia ya leo inakumbwa na machafuko na ukosefu wa mantiki, huku biashara ya silaha, vurugu, na kiburi cha madaraka vikishamiri.

“Nguvu ya mataifa sasa hupimwa kwa uwezo wao wa kuharibu ubinadamu na kiwango cha uharibifu wanachoweza kusababisha, kiasi kwamba maisha ya wasio na hatia hayana thamani tena. Haya yote yanatokana na kupuuzwa kwa maadili ya kidini na kiutu, juhudi za kuyatenga na maisha ya kijamii, na kudhoofishwa kwa nafasi yao ya kuwaongoza watu kuelekea wema na huruma.”

Alisisitiza kuwa Al-Azhar imejikita katika kueneza ujumbe wa amani na udugu, na kujitolea kwa ajili ya wanyonge na wahitaji.

Pia alieleza kuwa dunia ya leo inahitaji kwa dharura kujenga utamaduni wa mazungumzo ya kidini, na kuthibitisha kuwa dini hazipingani wala kupigana kama wengine wanavyodai kwa upotoshaji.

“Kinyume chake, dini huingia katika mazungumzo na hukubaliana juu ya wajibu wa kusimamisha amani kwa wote, bila kujali dini, rangi, au asili.”

Mwisho wa kikao hicho, Sheikh al-Tayyib alimwomba Naibu Katibu Mkuu wa Vatican kufikisha mwaliko wake kwa Papa Leo XIV kuitembelea Al-Azhar.

3495237

captcha