Jumla ya watoto wa kiume na wa kike 1,030 walienziwa katika hafla hiyo, ambapo 600 kati yao ni wanafunzi wa Al-Azhar.
Sherehe hiyo ilifanyika katika kijiji cha Ghamza Al-Kubra, na kuhudhuriwa na maulamaa wakuu pamoja na maafisa wa Al-Azhar.
Hii ni sehemu ya sherehe kubwa ya kila mwaka inayowatukuza wahifadhi wa Qur’ani, kwa juhudi za Kituo cha Kiislamu cha “Imam” chini ya usimamizi wa Sheikh Mkuu wa Al-Azhar, Ahmad el-Tayeb.
Rais wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar, Salama Juma Dawood, alikuwa miongoni mwa waliohudhuria. Katika hotuba yake, aliwapongeza wahifadhi wa Qur’ani pamoja na familia zao, na kusisitiza kuwa dhamira ya Al-Azhar ni kuhifadhi turathi za Uislamu na Waislamu.
Aliongeza kuwa wahifadhi wa Qur’ani ni watumishi maalum wa Mwenyezi Mungu, na Qur’ani Tukufu imebeba sifa ya Mola Mlezi, mojawapo ya majina mazuri kabisa — Al-Karim.
Dawood alisisitiza: “Tunachoshuhudia leo ni matunda halisi ya sera ya Al-Azhar inayojikita katika kuhifadhi Qur’ani na Sunnah safi ya Mtume (rehema na amani zimshukie).”
Aliongeza kuwa Ummah wa Kiislamu, mradi tu kuna wahifadhi wa Qur’ani ndani yake, daima utakuwa mshindi na uliohifadhiwa.
Sherehe ilihitimishwa kwa kutolewa zawadi ya safari 210 za Umrah kwa wahifadhi bora wa kiume na wa kike waliokamilisha kuhifadhi Qur’ani yote, pamoja na zawadi za fedha kwa wahifadhi wengine.
/3495252